31 Machi 2025 - 22:12
Source: Parstoday
Mamia ya Waislamu wahofiwa kufariki katika tetemeko la ardhi Myanmar

Mamia ya Waislamu wanahofiwa kuwa miongoni mwa watu zaidi ya 1,600 waliopoteza maisha katika tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katikati ya Myanmar, wakati walipokuwa wakiswali misikitini katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (ya kivuli) iliyo uhamishoni, zaidi ya misikiti 50 nchini humo iliharibiwa wakati tetemeko lenye ukubwa wa kipimo cha 7.7 lilipopkumba nchi hiyo siku ya Ijumaa.

Htet Min Oo ni miongoni mwa Walioshuhudia tetemeko hilo. Anasema alikuwa akifanya wudhu kabla ya sala katika msikiti karibu na nyumba yake huko Mandalay. Nyumba yake ilianguka pamoja na sehemu ya msikiti huo, na nusu ya mwili wake ulinaswa chini ya kifusi cha ukuta uliowazika shangazi zake wawili. Anasema kuwa wakazi walikimbilia kuwaokoa, lakini ni mmoja tu aliyeokoka.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 25 aliambia shirika la habari la Reuters kuwa wajomba zake wawili pamoja na bibi yake pia walikuwa wamekwama chini ya vifusi vya saruji. Bila vifaa vizito, alijaribu kwa juhudi zote kuondoa kifusi kwa mikono yake lakini hakuweza.

Mwananchi mwenye umri wa miaka 39 kutoka eneo la Mandalay ameeleza hali ya kusikitisha alipojaribu kumuokoa mwanaume aliyenaswa chini ya kifusi cha msikiti ulioporomoka katika kijiji cha Sule Kone, lakini alilazimika kukimbia kutokana na matetemeko ya baada.

 Amesema watu 10 waliuawa , wakiwa miongoni mwa 23 waliokufa katika misikiti mitatu iliyoharibiwa kijijini humo. Alieleza kuwa pingamizi ya serikali ilizuia misikiti hiyo kuboreshwa.

Waislamu ni wachache katika nchi ya Myanmar inayotawaliwa na Wabudha walio wengi, na wamekuwa wakikandamizwa na kutengwa na serikali mfululizo, huku makundi ya kitaifa yenye misimamo mikali yakichochea vurugu miaka ya hivi karibuni.

Waislamu wa Rohingya, kundi kubwa la wachache, ni miongoni mwa walioteswa sana na mamlaka za Myanmar, wakikumbwa na vifo vya halaiki na kufukuzwa.

Kwa miongo kadhaa, serikali ya Myanmar mekuwa ikizuia Waislamu kupata vibali vya kukarabati au kujenga misikiti. Taarifa zinasema misikiti ya kihistoria imeharibika kwa sababu matengenezo ya kawaida hayakuruhusiwa.

Hadi sasa, tetemeko hilo pia limeharibu majengo mengine, madaraja, na barabara katika maeneo mengi ya Myanmar.

Hata hivyo, wengi wanaamini ukubwa halisi wa janga hilo bado haujafahamika kwa sababu ya mawasiliano duni katika maeneo ya mbali.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha