3 Aprili 2025 - 18:16
Source: Parstoday
Trump atafakari pendekezo la mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran

Ikulu ya Marekani White House inatathmini pendekezo la kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran; na wakati huo huo inaongeza kiwango cha vikosi vya jeshi lake vamizi katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ili kujiandaa kwa operesheni tarajiwa za kijeshi dhidi ya Tehran.

Tovuti ya habari ya Axios yenye makao yake mjini Virginia imenukuu maafisa wawili wa Marekani ambao hawakutajwa majina wakisema katika ripoti yake ya jana Jumatano kwamba, "Utawala wa Trump unadhani mazungumzo ya moja kwa moja yatakuwa na nafasi kubwa ya kufaulu lakini haiondoi muundo ambao Wairani walipendekeza na haupingi Oman kuwa mpatanishi kati ya nchi hizo, kama ambavyo nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi ilivyokuwa huko nyuma," mmoja wa maafisa alisema.

Maafisa hao wawili wa Marekani wanaofahamu majadiliano ya ndani ya Ikulu ya White House wameiambia Axios kwamba, hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa, na kwamba utawala wa Trump unazingatia pendekezo la Iran la mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.

Axios imeripoti hayo na kuongeza kuwa, Trump ameashiria nia ya kufikia makubaliano mapya na Iran kuchukua nafasi ya mapatano ya JCPOA ambayo kiongozi huyo wa US alichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa kwayo katika muhula wake wa kwanza, lakini ameonya kuwa kutofikiwa mapatano kutazusha "mashambulizi ya mabomu" (dhidi ya Iran).

Jumamosi iliyopita, Trump katika mahojiano na NBC News alisema kuwa, Iran itashambuliwa kwa mabomu iwapo haitafikia makubaliano na Marekani.

Iran imelaani vikali vitisho hivyo vya Trump vya kuishambulia nchi hii kijeshi, ambapo imevitaja kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha