Ali Bahraini, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa huko Geneva amewasilisha malalamiko yake wakati wa kupitishwa kwa rasimu ya azimio L.20 lenye anuani ya “Hali ya Haki za Binadamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran” katika kikao cha 58 cha Baraza la Haki za Binadamu. Amekosoa vikali mifumo ya uangalizi ya kibaguzi na isiyo ya haki iliyowekwa katika azimio hilo dhidi ya Iran.
Aidha amesisitiza kuwa hatua hiyo inaliingiza Baraza hilo katika mtego mpya wa kutofanya kazi ipasavyo na upotevu wa rasilimali, na hivyo kupunguza imani kwa taasisi hiyo.
Mwakilishi huyo wa kudumu wa Iran mjini Geneva, akizungumzia namna utawala wa Kizayuni wa Israel unavyokiuka haki za binaaadamu za Wapalestina na pia namna viongozi wa utawala huo waliovyokweka adhabu, amesema:“Wakati ambapo ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unafanyika kila mara katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, na wahusika wake wakiwa na kinga ya juu kabisa dhidi ya adhabu, waandaaji wa rasimu ya azimio L.20 wanajaribu kupotosha baraza hili kwa kuonyesha taswira isiyo sahihi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran.”
Bahraini amesisitiza juu ya historia ya kitamaduni ya Iran na kusema:“Iran, kama nchi yenye historia na ustaarabu wa muda mrefu, daima imejivunia mafanikio yake kwa ajili ya ubinadamu. Nchi yetu imepitia milima na mabonde mengi na haishangazwi na mashinikizo kama haya. Kwa hivyo, inawaonya waandaaji wa azimio hili na wahusika wakuu wa maigizo haya ya kisiasa kuwa watawajibika kwa dhuluma hizi dhidi ya watu wa Iran na ubinadamu kwa ujumla.”
Mwisho, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa huko Geneva amewaalika waliokuwa kwenye kikao hicho kuhudhuria onyesho la muziki wa Iran linalotolewa na kundi la “Sorush-e-Mowlana”, litakalofanyika Ijumaa tarehe 4 Aprili 2025 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, mbele ya kikao cha Baraza la Haki za Binadamu, ili kufurahia ladha na sanaa ya kale ya Kiirani.
342/
Your Comment