4 Aprili 2025 - 23:14
Source: Parstoday
Rais Pezeshkian: Iran haiko vitani na nchi yoyote

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia na kusisitiza kwa kusema: "Nina imani kwamba kama nchi za Kiislamu zitafanya kazi kwa pamoja, zinaweza kuleta usalama na ustawi bora katika eneo hili."

Katika mazungumzo hayo ya usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Rais Pezeshkian amempongeza Mohammad Bin Salman na taifa la Saudi Arabia kwa mnasaba wa sherehe za Sikukuu ya Idul Fitr na kusema kuwa, mwezi mtukufu wa Ramadhani ulikuwa ni fursa bora ya kukumbuka mambo ya pamoja ya Waislamu ikiwemo Qur'ani Tukufu na ibada za mwezi huo mtukufu. Amesema: Nchi za Kiislamu zinaweza kujiletea amani, usalama na maendeleo ya hali ya juu kwa kutegemea mambo hayo ya pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano baina yao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Rais Pezeshkian amesema, iwapo Waislamu watashikana mikono na kuwa kitu kimoja, wanaweza kuzuia dhulma na jinai dhidi ya baadhi ya nchi za Kiislamu, zikiwemo Palestina na watu wa Ghaza. Amesema: "Nina imani kuwa nchi za Kiislamu kwa kushirikiana, zinaweza kuleta usalama na ustawi bora katika eneo hili."

Akimshukuru Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia kuhusu matamshi na msimamo wake wa ushirikiano na mshikamano baina ya Waislamu na nchi jirani za eneo hili, Pezeshkian amesema: "Kama ulivyosema katika hotuba yako, iwapo nchi za Kiislamu zitashikamana, zinaweza kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Ghaza na kuleta utulivu na amani na hatimaye kufanya kazi kwa ajili ya ustawi zaidi wa eneo hili."

Katika mazungumzo hayo ya simu, Mwanamfalme wa Saudia naye ametoa pongezi zake za Idul Fitr kwa Rais na taifa la Iran na amemshukuru na kumpongeza Rais Pezeshkian kwa ubunifu wake wa kuimarisha mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Amesema: "Ninatumai kwamba kwa kuendeleza mchakato wa kuimarisha ushirikiano kati yetu, tunaweza kupata mafanikio zaidi katika masuala ya utulivu, usalama na ustawi wa ukanda huu mzima."

Mohammed bin Salman Al Saud akitoa uchambuzi wa hali ya mambo katika eneo na nchi za Kiislamu amebainisha kuwa: Ushirikiano kati ya Iran, Saudi Arabia na nchi nyingine za eneo unaweza kuchangia ipasavyo katika kuimarisha utulivu na kusimamisha amani. Amesema: Saudi Arabia iko tayari kuchukua jukumu la kusaidia kutatua mvutano wowote na ukosefu wa usalama katika eneo hili.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha