Licha ya vitisho na mashambulizi ya pamoja ya kijeshi ya Wamarekani, Waingereza na Wazayuni, jeshi la Yemen linaendeleza operesheni zake katika Bahari Nyekundu na dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Wanamuqawa wa Yemen na jeshi la nchi hiyo wanasisitiza kuwa wataendeleza oparesheni zao dhidi ya Marekani na Wazayuni hadi hapo utawala wa Kizayuni utapositisha jinai zake dhidi ya watu wa Palestina.
Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza kuwa: Wanajeshi wa kikosi cha makombora na ndege zisizo na rubani vya Yemen wamepigana na kukabiliana katika eneo la kaskazini mwa Bahari Nyekundu na meli kadhaa za kivita za Marekani ikiwemo meli ya USS Harry Truman inayobeba ndege za kivita. Brigedia Jenerali Yahya Saree ameeleza kuwa mapigano hayo yaliendelea kwa sasa kadhaa na yamefanyika kwa kutumia makombora ya cruise, balistiki na droni kadhaa. Saree ameongeza kuwa: Jeshi la Wanamaji la Yemen limepiga meli ya Marekani ya Harry Truman kwa kombora la balistiki.
Mashambulizi ya anga ya ndege za kivita za Marekani yangali yanaendelea dhidi ya Yemen na hadi sasa yameuwa na kujeruhi makumi ya watu.
Ndege za kivita za Marekani juzi Jumamosi pia zilifanya mashambulizi mara mblili katika eneo la Kohlan mashariki mwa mkoa wa Sa'ada, kaskazini mwa Yemen. Hii ni katika hali ambayo shirika rasmi la habari lal Yemen limekadhibisha madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kushambuliwa viongozi na makamanda wa kijeshi wa nchi hiyo.
Katika miezi ya karibuni jeshi la Yemen limekuwa likizuia au kuzishambulia kwa makombora meli zote zinazovuka katika Bahari Nyekundu kuelekea Israel ili kukomesha mashambulizi ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza. Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuendelea kushambulia meli za utawala wa Kizayuni au zile zinazoelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu katika Bahari Nyekundu hadi pale utawala wa Israel utakapositisha mashambulizi yake dhidi ya Gaza.
Utawala wa Kizayuni unaosaidiwa na kuungwa mkono kikamilifu na nchi za Magharibi, unaendeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina, na kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu duniani mkabala wa jinai kubwa za Israel kimeutia kiburi utawala huo haramu cha kuendeleza mauaji dhidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina.
Marekani na muitifaki wake wa siku zote, yaani Uingereza, pia zinaendelea kuuhami utawala wa Kizayuni licha ya kupingwa na nchi za kanda hii na wanaharakati wa kisiasa na makundi yanayounga mkono amani katika ulimwengu wa Magharibi; na hivyo kuendeleza hatua zao za kuibua mivutano katika Bahari Nyekundu dhidi ya serikali ya Yemen.
Viongozi wa Marekani walidai kuwa mashambulizi yao ya kijeshi yamesitisha oparesheni za jeshi la Yemen lakini hali katika Bahari Nyekundu ni kinyume na madai yao hayo.
Ukweli ni kwamba, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimebadili mlingano wa nguvu katika Bahari Nyekundu kwa maslahi ya nchi hiyo, na wanajeshi vamizi wa Marekani pia wanatekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen katika jitihada zilizofeli za kujaribu kurudisha hadhi na haiba yao iliyotoweka.
Pamoja na hayo, tunapasa kuashiria ukweli kwamba, mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani na washirika wake katika eneo hili kwa lengo la kuuhami tawala wa Kizayuni wa Isarel, si tu kuwa hayana taathira katika kukabiliana na jeshi la Yemen, bali kwa namna fulani, yanadhihirisha jinsi Washington inavyoendelea kushiriki katika mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina na kuuhami kwa hali na mali utawala ambao viongozi wake wanasakwa na mahakama za kimataifa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na jinai dhidii ya binadamu.
342/
Your Comment