Siku ya Jumatatu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Huduma za Mradi UNOPS, Jorge Moreira da Silva, aliungana na wakuu wa OCHA, UNICEF, UNRWA, WFP, WHO na IOM kutoa taarifa ya pamoja kuhusu hali mbaya sana ya kibinadamu inayoendelea kushuhudiwa huko Ghaza.
Mashirika hayo ya UN yametoa indhari juu ya uhaba mkubwa wa misaada na baa la njaa lililotanda katika eneo hilo tangu jeshi la Israel lianzishe tena mashambulio ya kinyama ya kila upande mnamo Machi 18.
Katika taarifa yao hiyo ya pamoja kwa vyombo vya habari, wakuu wa mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa wamesema, kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, hakuna vifaa na bidhaa za kibiashara au za kibinadamu zilizoingia Ghaza baada ya Israel kuzuia kikamilifu kuingia malori ya misaada.
Wamefafanua kwa kusema: "zaidi ya watu milioni mbili na laki moja wamekwama, wanapigwa mabomu na kuteswa tena kwa njaa, wakat, katika maeneo ya vivuko, chakula, dawa, mafuta na vifaa vya makazi vinarundikana, na vifaa muhimu vimekwama".
Mashirika hayo yameongeza kuwa watoto wapatao 1,000 waliuawa au kujeruhiwa katika wiki ya kwanza baada ya kuanza tena mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel, ambayo ni idadi kubwa zaidi ya watoto waliouawa ndani ya muda wa wiki moja katika mwaka uliopita.
Huku yakiielezea hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza kuwa ni mbaya sana kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa, mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yamesema, eneo hilo linashuhudia vitendo vya vita "vinavyoonyesha kutojaliwa hata chembe maisha ya binadamu".
Mnamo Machi 18, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha tena vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na kuvunja kikamilifu usitishaji mapigano uliodumu kwa miezi miwili kufuatia makubaliano uliyofikia na harakati ya Hamas kwa upatanishi wa serikali iliyopita ya Marekani, Qatar na Misri.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ghaza, Wapalestina wapatao 1,391 wameuawa shahidi na wengine 3,434 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha tena mashambulio hayo ya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo.../
342/
Your Comment