10 Aprili 2025 - 19:57
Source: Parstoday
Russia: Dunia imechoshwa na vitisho visivyokwisha vya Marekani dhidi ya Iran

Russia imelaani vikali vitisho vya mara kwa mara vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema dunia imechoshwa na hali hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, alisema siku ya Jumatano kwamba. “Mataifa duniani yameanza kuchoshwa na vitisho visivyokwisha dhidi ya Iran."

Ameongeza kuwa: “Uchovu huu unaambatana na ukosefu wa uelewa juu ya kwa nini suala hili, ambalo tayari lilipata suluhu ya kidiplomasia iliyosainiwa kihalali, linaendelea kutumiwa kama kisingizio cha uwezekano wa uchokozi wa kijeshi."

Kauli hiyo ilijikita hasa kwenye vitisho vilivyotolewa karibuni  na  Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran iwapo hakutapatikana makubaliano ya pamoja.

Iran na Marekani zinatarajiwa kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Oman tarehe 12 Aprili, kwa lengo la kupunguza mvutano uliodumu kwa miaka mingi.

Zakharova ameonya kuwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran hayataleta amani, na hivyo amebainisha matumaini kuwa mazungumzo yajayo yatasaidia kuzuia mgogoro.

Aidha, Zakharova amekosoa mtazamo wa mataifa ya Magharibi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, akitilia shaka dhamira yao ya kweli ya kutafuta suluhu ya mvutano huo wa muda mrefu.

“Kwa ujumla, namna wenzetu wa Magharibi walivyoshughulikia suala hili hadi sasa, inazua mashaka kama kweli wana nia ya dhati ya kuutatua mgogoro huu.”

Zakharova pia alisema kuwa Tehran haiwezi kubeba lawama kwa madhara yaliyosababishwa na “matendo haramu ya wale ambao, kwa upofu wa kisiasa na makadirio potofu, walidhoofisha makubaliano.”

Mnamo mwaka 2018, wakati wa urais wa kwanza wa Donald Trump, Marekani ilijiondoa kwa upande mmoja kutoka kwenye Makubaliano ya Nyuklia ya Pamoja (JCPOA), mkataba ulioweka mipaka kwenye shughuli za nyuklia za Iran, kuruhusu ukaguzi zaidi, na kupunguza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo.

Kwa upande mwingine, Dmitry Peskov, msemaji wa  Kremlin, Ikulu ya Rais wa Russia , amesisitiza umuhimu wa diplomasia na mazungumzo badala ya hatua zinazoweza kuongeza mivutano.

Amesema: “Ni wakati wa kuwekeza kwenye diplomasia badala ya kulimbikiza vitisho vinavyoweza kupelekea hali ya kutoaminiana na hatimaye machafuko."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha