11 Aprili 2025 - 18:34
Source: Parstoday
Mamilioni waandamana Yemen kuunga mkono Ghaza

Mamilioni ya wananchi wa Yemen wamemiminika mitaani katika mkoa wa Sa'ada leo Ijumaa na kufurika katika viwanja 35 vya mkoa huo wa kaskazini ya Yemen chini ya kaulimbiu ya "Jihadi, Uthabiti na Ushujaa... Hatutaiacha peke yake Ghaza."

Maandamano makubwa zaidi yamefanyika katika Uwanja wa Maulidun Nabawi magharibi mwa mji wa Sa'ada, wakati maandamano mengine yamefanyika katika viwanja vingine 34 vya mkoa huo. 

Maandamano mengine ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina yamefanyika pia leo mchana katika viwanja vya Al-Khamis huko Manbeh, Shada, Al-Jafrah, na Udlah huko Al-Hashwa na Al-Thabit huko Qataber ili kuonesha uungaji mkono usio na kifani wa wananchi wa Yemen kwa ndugu zao Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza.

Waandamanaji wamenyanyua juu bendera za Yemen na Palestina pamoja na mabango ya ukombozi na ya kulaani hujuma ya Wazayuni na Marekani dhidi ya Palestina na Yemen, na kuthibitisha uimara wa msimamo wa Yemen katika kuwaunga mkono Wapalestina na kukabiliana uchokozi wa Marekani dhidi ya nchi yao.

Katika maandamano hayo, waandamanaji wamesoma kwa sauti kubwa na kwa pamoja mashairi maarufu yakithibitisha uungaji mkono wa wananchi wa Yemen kwa Palestina, upinzani wao dhidi ya kiburi na ukandamizaji wa Marekani na kusimama kidete mbele ya jinai za maadui hadi ushindi kamili upatikane.

Wamesisitiza kuwa, hujuma ya Marekani dhidi ya Yemen inalenga kuwazuia wananchi Waislamu wa nchi hiyo kusimama bega kwa bega na ndugu zao Wapalestina na kusisitiza kuwa, uchokozi huo hautoweza kuiondoa Yemen kwenye msimamo wake, na kwa vile haikuweza kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mingi iliyopita kupitia mamia ya maelfu ya mashambulizi ambayo iliyafanywa dhidi ya Yemen, hivi sasa pia haitaweza kuzuia chochote. Vile vile wamesisitiza kuwa uchokozi wa Marekani utaongeza tu uimara wa watu wa Yemen wa kupigania haki na kupinga dhulma.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha