11 Aprili 2025 - 18:35
Source: Parstoday
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina yapongeza uamuzi wa Macron kuitambua rasmi Palestina

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imekaribisha msimamo uliotangazwa na Rais wa Ufaransa kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kulitambua rasmi Taifa la Palestina katika miezi ijayo.

Ikiashiria habari hii, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetangaza kuwa: "Tunakaribisha matamshi ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusu kutambuliwa rasmi Taifa la Palestina katika miezi ijayo."

Taarifa ya wizara hiyo imesisitiza kuwa: "Tunatambua msimamo huu wa Ufaransa kuwa ni hatua ya kuunga mkono suluhisho la amani."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina pia imezitaka nchi ambazo bado hazijalitambua taifa la Palestina zikiwemo nchi za Ulaya kupiga hatua katika njia hiyo. Vilevile imetoa wito wa kuungwa mkono juhudi za Palestina za kupata uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa kusitishwa mara moja mauaji ya kimbari, mpango wa kulazimishwa Wapalestina kuhama makazi yao, na kughusubiwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ni muhimu katika mchakato wa kurejesha usalama na utulivu katika eneo la Asia Magharibi.

Hapo awali, Rais wa Ufaransa alisema kuwa Paris inaweza kutambua rasmi nchi huru ya Palestina mwezi Juni mwaka huu.

"Nataka kuelekea katika kulitambua rasmi taifa la Palestina. Sitafanya hivi ili kumfurahisha huyu au yule, lakini kwa sababu itakuwa hatua ya kiadilifu", amesema Emmanuel Macron.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha