Kufukuzwa kazi kwa askari hao wa akiba kunadhihirisha kuongezeka kwa mpasuko ndani ya vyombo vya kijeshi na kisiasa vya utawala wa Kizayuni kutokana na kushindwa kufikia malengo ya kistratijia huko Gaza, licha ya miezi kadhaa ya uchokozi wa kikatili unaoungwa mkono na Marekani ambao umesababisha maelfu ya raia wa Palestina kuuawa na kuyakimbia makazi yao.
Yair Golan, mkuu wa eti "Chama cha Demokrasia" na afisa wa zamani wa kijeshi wa Israel, amelaani kitendo cha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kukataa kubeba dhima ya mgogoro wa sasa wa kiusalama wa utawala huo ghasibu, na kufeli kutoa kipaumbele kwa suala la kuachiliwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza.
Golan amesema kuwa, wale waliotia saini waraka huo wa malalamiko ni watetezi wa kweli wa utawala huo, na wala sio wasaliti na wahaini. Hii ni katika hali ambayo, Kamandi ya Amri ya jeshi la utawala huo pandikizi imeitaja hatua ya askari hao wa akiba kama "usaliti wa uaminifu."
Hii ni katika hali ambayo, mvutano mkubwa unazidi kutokota ndani ya baraza la mawaziri la Netanyahu kutokana na kushindwa kufikia malengo yake ya vita yaliyotangazwa, yaani, kutokomezwa kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas na kuachiliwa huru mateka Waisraeli.
Aidha haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Fedha wa wa Israel, Bezalel Smotrich, kutangaza kujiuzulu kutoka wadhifa wake, jambo ambalo linaongeza matatizo ndani ya serikali ya muungano ya Netanyahu.
342/
Your Comment