Jinai hiyo ya Marekani imefanywa katika soko lililojaa watu katika kitongoji cha al-Farwa kilichoko kwenye wilaya ya Sha'ub alfajiri ya kuamkia leo.Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu watu wengi wangali wamenasa chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa katika shambulio hilo.
Maeneo mengine ya Sana'a, ikiwa ni pamoja na Attan na Wilaya ya al-Wahda, nayo pia yamelengwa na mashambulizi ya kinyama ya anga ya Marekani alfajiri ya kuamkia leo.Sambamba na hayo, mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani yamelenga maeneo kadhaa ya mkoa wa Sa'ada, kaskazini mwa Yemen, eneo la kati la Ma'rib, na Hudaydah magharibi.
Siku ya Jumapili pia, raia wasiopungua watatu waliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Marekani yaliyolenga mji mkuu Sana'a.Kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen, ikinukuu taarifa ya Wizara ya Afya ya Umma na Idadi ya Watu imetangaza kuwa Jumamosi usiku, jeshi la Marekani lilianzisha mashambulizi 21 ya anga dhidi ya Sana'a pamoja na viunga vyake vya magharibi, mashariki na kusini.
Jeshi la Marekani limekuwa likifanya mashambulizi karibu kila siku dhidi ya Yemen kwa muda wa mwezi mmoja sasa likidai kuwa mashambulizi hayo yanalenga kusimamisha operesheni za kijeshi za harakati ya Ansarullah dhidi ya meli zenye uhusiano na Israel.
Jeshi la Yemen hata hivyo limesema halitasimamisha mashambulizi yake dhidi ya meli zinazoelekea kwenye bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel hadi pale utawala huo ghasibu utakapositisha jinai zake dhidi ya Ukanda wa Ghaza.../
342/
Your Comment