22 Aprili 2025 - 22:48
Source: Parstoday
Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti wa Al Aqsa, eneo lake lafanana na 'kambi ya kijeshi'

Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena ua wa Msikiti wa Al-Aqsa huku wakisindikizwa na polisi wa utawala ghasibu wa Israel Baitul Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Wafa, mashuhuda wa tukio hilo wamesema, walowezi hao wa Kizayuni walifika kwa vikundi na kuzurura katika eneo hilo kwa madhumuni ya kuwachochea na "kuwachokoza" Wapalestina.

Wafa imeendelea kueleza kuwa, wakati wa uvamizi huo, vikosi vya jeshi la polisi la utawala wa Kizayuni Israel vilisambazwa kwa wingi katika eneo la kale la mji wa Quds, vikiwaweka askari wake katika kila lango linaloelekea Al-Aqsa. Mashuhuda wamelieleza shirika hilo la habari la Palestina kwamba eneo hilo la Msikiti wa Al-Aqsa linaoekana kama "kambi ya kijeshi".

Polisi wa Kizayuni waliweka vizuizi vikali kwa Wapalestina waliojaribu kuingia msikitini, na kuwazuia wengi wao kuingia kwenye eneo hilo.

Hujuma dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa zinafanyika katika hali ambayo, walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya chuki walisambaza kwenye mitandao ya kijamii video iliyotengenezwa kwa kutumia Akili Mnemba (AI) yenye anuani "Mwaka Ujao huko Jerusalem". Video hiyo inaonyesha Msikiti wa Al-Aqsa ukiripuliwa na mahala pake kujengwa kile kinachoitwa 'Hekalu la Tatu'.

Hatua hiyo ya kichochezi ya walowezi hao wa Kizayuni imelaaniwa vikali kikanda na kimataifa.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha