23 Aprili 2025 - 23:35
Source: Parstoday
Guterres: Mama Dunia anaugua homa

Wakati kiwango cha joto duniani kinakuwa ni cha juu na hakuna dalili za kiwango hicho kushuka, ndipo kiwango hicho kinafananishwa na ‘homa kali’, na hivyo sasa tunaweza kusema kwamba ‘Mama Dunia anaugua homa.

Hivyo ndivyo aonavyo António Guterres, Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa na kuweka bayana kwenye ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia iliyoadhimishwa Aprili 22, 2025.

Guterres amesema tiba ya homa hiyo haiko mbali, akisema ni kupunguza haraka utoaji wa hewa chafuzi na kuongeza kasi ya mabadiliko ili kumlinda sio tu Mama Dunia, bali pia kulinda binadamu wanaoishi ndani ya sayari hiyo.

Katibu Mkuu amesema dalili za ‘homa’ kali inayokumba dunia ziko dhahiri: mioto ya nyika inayosababisha uharibifu mkubwa, mafuriko na joto kupindukia. Watu wanapoteza maisha, halikadhalika mbinu zao za kujipatia kipato zinasambaratishwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP linataja visababishi vya homa kali inayokumba dunia kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na binadamu, uhalifu unaoharibu bayonuai ikiwemo ukataji miti hovyo, binadamu kubadili matumizi ya ardhi, kilimo cha kupindukia kisichojali mazingira, ufugaji holela, biashara haramu ya wanyamapori na matumizi ya nishati kisukuku.

Katibu Mkuu anasema kwamba majawabu yanayopendekezwa na wanasayansi ni majawabu ambayo sio tu ni rahisi bali pia ni ya kiafya kwa mazingira na binadamu na pia ni salama.

Majawabu hayo ni pamoja na matumizi ya nishati rejelezi kama vile sola moja ya mbadala wa nishati kisukuku.

Halikadhalika hatua za kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kujenga uchumi bora na salama kwa jamii kwa zama za sasa na zama zijazo.

Hivyo amesema, “mwaka huu ni muhimu sana. Nchi zote lazima ziandae mipango mipya ya kitaifa ya hatua kwa tabianchi, mipango inayoendana na kudhibiti kiwango cha joto duniani kisiongezeke kwa zaidi ya nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi –kwani kipimo hicho kikizingatiwa kitaepusha janga baya zaidi tabianchi.”

Guterres amesema wakati huu ni fursa muhimu ya kunufaika na nishati salama na safi. “Ninasihi nchi zote zitumie fursa hii, huku kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, G20 zikiongoza njia.”

Amesema kinachohitajika pia ni hatua za kudhibiti uchafuzi, kuondokana na kupoteza biyonuai na kupatia nchi ufadhili unaohitaji ili kulinda sayari dunia.

Katibu Mkuu ametamatisha kwa kusema: “Kwa pamoja hebu tufanya kazi ili mwaka 2025 uwe mwaka wa kurejesha afya kwa Mama Dunia.”

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha