25 Aprili 2025 - 22:43
Source: Parstoday
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Mazungumzo na Marekani yanaendelea kwa tahadhari

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, Hujjatul-Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu-Torabi Fard amesisitiza kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanafanyika kwa tahadhari na kutoka kwenye nafasi yenye nguvu na heshima.

 Akihutubia maelfu ya waumini katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, Sayyid Mohammad Hassan Abu-Torabi Fard, ameashiria mwanzo wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ambayo yameanza kwa ombi la mamlaka ya juu kabisa ya Marekani ndani ya mfumo wa kanuni na sheria ulioainishwa na Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Mazungumzo haya yanaendelea kwa tahadhari, umakini na kwa jicho la shaka, kwa kuzingatia historia ya Marekani kukiuka makubaliano hususan kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018."

Sayyid Abu-Torabi Fard ameongeza kuwa: "Katika miongo ya hivi karibuni, mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umekuwa kisingizio cha mashinikizo ya Marekani, lakini kurejeshwa vikwazo vya juu zaidi, ingawa kumetuweka chini ya mashinikizo, kumetufunza kwamba ni lazima kutumia uwezo kamili wa nchi kukabiliana na changamoto na vikwazo vya kiuchumi, bila kutegemea ahadi za Magharibi."

Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria misimamo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusiana na mazungumzo hayo na kusema: "Waziri wa Mambo ya Nje ameyataja mazungumzo ya Muscat kuwa ni mtihani mwengine wa kuipima Marekani na akasisitiza kuwa kuondolewa kikamilifu vikwazo na kupewa dhamana ya kisheria kunaweza kuandaa mazingira mazuri ya mazungumzo."

Amesisitiza kuwa: "Mamlaka zote lazima, zitumie uwezo kamili wa nchi kubadilisha na kuboresha miundombinu ili kufikia ukuaji wa juu wa uchumi."

Katika khutba ya kwanza ya Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, Sayyid Mohammad Hassan Abu-Torabi Fard ametaja Hadithi zinazoeleza sifa na fadhila za mwezi wa Dhul-Qa'dah. Amemnukuu mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu, Sayyid Ibn Tawus, aliyetaja mwezi wa Dhul-Qa'dah kuwa ni wakati mwafaka wa kuomba dua wakati wa matatizo. Amewahimiza Waislamu kuomba dua ya kuondolea dhulma, hasa kwa watu waliodhulumiwa wa Gaza huko Palestina.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha