1 Mei 2025 - 23:36
Source: Parstoday
Trump na Gorbachev; Je, historia inajirudia huko Marekani?

Gazeti la kila wiki la Marekani la Newsweek limeripoti kuhusu mbinu mahususi zinazotumiwa na Rais wa nchi hiyo, Donald Trump katika sera za kigeni.

Makala hiyo iliyotayarishwa kwa mnasaba wa kutimia siku mia moja za utawala wa Trump imeashiria mifano ya uzushi ambao Trump ameanzisha katika sera za kigeni za Marekani na kuandika: "Katika siku 100 za kwanza za uongozi wake, Donald Trump ametumia fursa zote kubadilisha uhusiano wa Marekani na mataifa mengine duniani." Ripoti ya Newsweek inasema: Trump amelishutumu tena Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kwa matumizi mabaya ya fedha za Marekani na kukosoa kiasi cha fedha ambacho Washington inatumia katika vita vya Ukraine.

Ripoti hiyo inaongeza kusema: Ukosoaji huo umesababisha malumbano makali ya maneno baina ya Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy mwezi Februari, ambapo Trump alimtuhumu Zelenskyy kuwa "anacheza kamari ya kuanzisha Vita vya Tatu vya Dunia".

Trump na Gorbachev; Je, historia inajirudia huko Marekani?

Ripoti hiyo inaendelea: Kwa upande mmoja, utawala wa Trump umekubali kufanya mazungumzo ya amani na Rais wa Russia, Vladimir Putin, na wakati huo huo umeanzisha vita vikali vya ushuru dhidi ya mshirika wake wa muda mrefu, Canada - pamoja na nchi zingine duniani- na unasisitiza mara kwa mara kwamba Canada lazima ijiunge na Marekani kama jimbo la 51 la nchi hiyo.

Mwishoni mwa ripoti yake, Newsweek imemnukuu Barry Scott Zellen, mtafiti na mtaalamu wa jiografia ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Connecticut, akisema: "Kipindi hiki cha urais wa Trump ni mojawapo ya myanzo ya kusisimua zaidi ya mihula ya urais tangu kipindi cha Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Soviet, lakini hatari zilizomkabili Gorbachev hatimaye zilisababisha mfumo wa Soviet sio tu kushindwa kufanya mageuzi, lakini pia kusambaratika. Barry Scott anamalizia kwa kuhoji: "Je, tutashuhudia tena hali kama hiyo huko Marekani?"

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha