10 Mei 2025 - 17:42
Kiongozi wa Mapinduzi ametoa uungaji mkono kamili kwa jamii ya wafanyakazi / Fikira zisikengeushwe kutoka kwenye suala la Palestina

Ayatollah Khamenei pia alisisitiza kuwa, pamoja na kuendelea kwa jinai na mauaji ya kikatili dhidi ya watu wa Gaza na Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani na Uingereza, mataifa yanapaswa kusimama dhidi ya utawala wa Kizayuni na wafuasi wake, na wasiruhusu masuala yanayohusu Palestina kusahaulika.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AhlulBayt (a.s) – ABNA: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Ali Khamenei, asubuhi ya leo amekutana na maelfu ya wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa mnasaba wa Wiki ya Kazi na Mfanyakazi. Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa utekelezaji wa kaulimbiu ya “Uwekezaji kwa Ajili ya Uzalishaji” unategemea sana kuwatambua wafanyakazi kuwa ni rasilimali kuu ya kazi na moja ya nguzo muhimu za uthabiti na uimara wa jamii.

Aidha, alieleza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa ajira na mazingira salama kwa wafanyakazi, kuwajengea ujuzi, na kuwashirikisha katika faida ya uzalishaji. Vilevile, alibainisha kuwa matumizi ya bidhaa na mali za ndani ya nchi yanapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa taifa, huku akisisitiza kuwa sambamba na kuendeleza utamaduni huo, ni lazima pia kuboresha ubora wa bidhaa za ndani.

Ayatollah Khamenei pia aligusia kuendelea kwa jinai na mauaji ya kikatili dhidi ya watu wa Gaza na Palestina yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani na Uingereza. Alisisitiza kuwa: “Mataifa yanapaswa kusimama dhidi ya utawala wa Kizayuni na washirika wake, na wasikubali suala la Palestina kusahaulika.

Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Khamenei, katika sehemu ya awali ya hotuba yake, alitoa pongezi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Ridha (a.s), na pia akamtaja kwa heshima Shahidi Rais Ebrahim Raisi, ambaye alikuwa na juhudi nyingi katika kushughulikia matatizo ya wananchi, hususan wafanyakazi.

Akimpongeza Waziri wa Masuala ya Hifadhi ya Jamii, Kazi, na Ushirikiano kwa hotuba yake katika mkutano huo, Ayatollah Khamenei alieleza kuwa maelezo aliyoyatoa kuhusu mapungufu na mahitaji ya mazingira ya kazi na jamii ya wafanyakazi yalikuwa sahihi na yanahitaji kupewa uangalifu na kufuatiliwa kwa dhati. Aliongeza kuwa: “Iwapo viongozi husika watajitahidi na kufanya maamuzi madhubuti, basi matatizo haya yanaweza kutatuliwa na ni jambo linalowezekana.”

Ayatollah Khamenei alieleza kuwa masuala ya kazi na wafanyakazi yana uhusiano wa moja kwa moja na hatima ya nchi. Akitilia mkazo thamani ya kazi na wafanyakazi, alisema: “Wafanyakazi wapendwa wanapaswa kujitambua thamani yao. Kupata riziki halali kwa njia ya uadilifu, bila uporaji au kula vya bure, pamoja na kuchangia katika mahitaji ya jamii kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma — haya ni mambo mawili ya thamani ya kiutu ambayo yanahesabiwa kuwa ni mema mbele ya Mwenyezi Mungu.”

Katika kufafanua thamani ya kazi, alisema: “Kazi ni nguzo kuu ya maisha ya binadamu. Bila kazi, maisha hukwama. Ingawa elimu na mitaji ni muhimu, hakuna hatua yoyote inayopigwa bila mfanyakazi. Ni mfanyakazi anayelipa uhai mitaji.”

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Uwekezaji kwa ajili ya Uzalishaji,” Kiongozi huyo alisisitiza kuwa wafanyakazi ndio mtaji mkuu wa uzalishaji na miongoni mwa nguzo muhimu za ustawi wa jamii. Aliongeza kuwa: “Uwekezaji wa kifedha hauwezi kufanikishwa bila irada na uwezo wa mfanyakazi.” Hivyo basi, alionya kuwa maadui wa jamii, wakiwemo wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu, tangu mwanzoni mwa Mapinduzi hadi leo, wamekuwa wakijaribu kuivuruga jamii ya wafanyakazi na kuwafanya wasikubali mazingira ya kazi ndani ya mfumo wa Kiislamu.

Ayatollah Khamenei pia alikumbusha kuhusu juhudi za vuguvugu la kikomunisti mwanzoni mwa Mapinduzi, ambazo zililenga kusimamisha na kuharibu uzalishaji. Alisema: “Hata leo, nia hiyo bado ipo, lakini wakati ule na sasa, wafanyakazi wetu wamesimama imara na wamewakabili kwa nguvu.”

Kuhusu kulinda thamani ya mfanyakazi, alisisitiza kuwa taasisi zote husika lazima zitekeleze wajibu wao ipasavyo. Akizungumzia usalama wa ajira, alisema: “Mfanyakazi anapaswa kuwa na uhakika kuhusu kazi yake ili aweze kupanga maisha yake, na asiishi kwa hofu ya kutegemea maamuzi ya watu wengine kuhusu ajira yake.”

Ayatollah Khamenei aliukosoa vikali mwenendo wa kufunga baadhi ya viwanda na vituo vya uzalishaji kwa kisingizio cha matatizo mbalimbali. Alisema: “Katika miaka ya nyuma, visingizio kama ukosefu wa malighafi au uchakavu wa mashine vilitumika, ilhali matatizo hayo yalistahili kutafutiwa suluhisho badala ya kufunga viwanda.”

Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Khamenei, alielezea wasiwasi wake kuhusu tabia ya kuuza ardhi zenye thamani kubwa za baadhi ya viwanda kwa ajili ya kupata faida ya haraka, huku shughuli za uzalishaji zikisitishwa na wafanyakazi kufutwa kazi. Alisisitiza:
“Taasisi za usimamizi, mahakama, pamoja na serikali kwa ujumla zinapaswa kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayajirudii.”

Ayatollah Khamenei aliipongeza serikali ya Shahidi Rais Ebrahim Raisi kwa juhudi zake katika kufufua takriban viwanda 8,000 vilivyokuwa vimefungwa au kufanya kazi kwa nusu uwezo. Alisema:
“Hatua hii ilithibitisha kuwa inawezekana kuzuia kufungwa kwa viwanda na kupungua kwa uwezo wa uzalishaji, jambo ambalo ni moja ya mafanikio ya kipekee ya shahidi huyo mpendwa.”

Katika kuzungumzia usalama wa ajira, alieleza mtazamo mwingine:
“Ni muhimu kuhakikisha usalama wa ajira sio tu kwa mfanyakazi bali pia kwa mjasiriamali. Haitakiwi kuwa mazingira ya uwekezaji yamsababishie mwekezaji hasara au hatari ya kupoteza mitaji yake.”

Ayatollah Khamenei alisisitiza pia umuhimu wa usalama wa kazini kwa wafanyakazi, akitaja kwa masikitiko ripoti za ajali nyingi katika migodi katika miaka ya hivi karibuni. Aliongeza:
“Hali ya usalama si tatizo la migodi tu. Usalama wa wafanyakazi katika vitengo vyote vya uzalishaji, iwe kupitia masharti ya kiufundi au kupitia mifumo ya bima na hifadhi ya jamii, ni suala la lazima linalopaswa kufuatiliwa kwa uzito.”

Aidha, alisisitiza kuwa moja ya majukumu muhimu kwa jamii ya kazi ni kuongeza ujuzi na weledi wa wafanyakazi. Alisema:
“Taasisi ya Ufundi Stadi na mafunzo yake ina mazingira mazuri ya kukuza ujuzi wa wafanyakazi. Pia mashirika makubwa yanaweza kuanzisha programu za mafunzo kandokando ya shughuli zao ili kuwajengea uwezo wafanyakazi wao.”

Akirejea kauli yake ya mara kwa mara kuhusu kusaidia uzalishaji wa ndani, Ayatollah Khamenei alisema:
“Kununua bidhaa za ndani ni msaada kwa mfanyakazi na mwekezaji wa Iran. Kinyume chake, kununua bidhaa za nje — ambazo zina mbadala wa ndani — ni kuwasaidia wafanyakazi na wawekezaji wa nje, jambo ambalo ni kinyume na haki na utu.”

Alisisitiza kuwa baadhi ya bidhaa za ndani zina ubora wa hali ya juu na akasema:
“Hebu tufanye hili kuwa utamaduni wa kitaifa — kwamba Muirani atumie bidhaa ya Iran, isipokuwa pale tu ambapo hakuna uzalishaji wa ndani kwa bidhaa hiyo.”

Ayatollah Khamenei alikosoa barua kutoka katika moja ya taasisi za serikali iliyopendekeza kuondoa marufuku ya uingizaji wa bidhaa ambazo tayari huzalishwa ndani ya nchi. Alisema kuwa kuruhusu uagizaji wa bidhaa hizo ni njia rahisi lakini yenye madhara kwa taifa na hasa kwa jamii ya wafanyakazi. Alisisitiza:
“Hata kama bidhaa ya ndani haina ubora wa kutosha, juhudini kuboresha ubora huo. Kama tulivyosema miaka iliyopita kwa wale waliokuwa wakilalamikia ubora wa magari ya ndani — kijana wa Iran, licha ya vikwazo vya kielimu na kiuchumi, anaweza kutengeneza kombora au bidhaa ambayo adui anakiri kwa heshima. Kwa hivyo, anaweza pia kutengeneza gari lenye ubora zaidi na matumizi kidogo ya mafuta.”

Kiongozi huyo alieleza kuwa moja ya hatua muhimu kwa manufaa ya wafanyakazi na waajiri ni kuwashirikisha wafanyakazi katika faida ya uzalishaji. Alisema:
“Mfanyakazi anapojua kuwa anashiriki katika faida ya bidhaa, hali hii huongeza motisha, huimarisha ubora na usahihi wa kazi, na kudumisha maisha ya kiwanda kwa miaka mingi.”

Ayatollah Khamenei alisisitiza pia juu ya umuhimu wa kutoa makazi kwa wafanyakazi kupitia vyama vya ushirika vya makazi au ujenzi wa nyumba za shirika karibu na maeneo ya viwanda.
Akiendelea, alizungumzia “utamaduni wa mahali pa kazi” na akaeleza:
“Katika falsafa ya Kimarx, mazingira ya kazi na maisha ni ya migongano na uadui; mfanyakazi anapaswa kumchukia mwenye kiwanda. Wazo hili batili liliipotezea dunia muda mwingi. Lakini katika Uislamu, kazi na maisha ni mazingira ya mshikamano, ushirikiano, na kuimarishana. Kwa hivyo, pande zote mbili mahali pa kazi zinapaswa kushirikiana kwa dhati kwa maendeleo ya kazi.”

Kiongozi huyo alifafanua kuwa mjadala kuhusu wafanyakazi haupaswi kupunguzwa hadi wale wa viwandani pekee. Alisema:
“Wafanyakazi wa ujenzi, mashambani, masoko ya matunda na mboga, pamoja na wanawake wanaojishughulisha na kazi za nyumbani kwa kutumia teknolojia mpya za mawasiliano kuuza bidhaa zao, wote wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la haki katika suala la hifadhi ya jamii na haki nyingine zilizotajwa.”

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatollah Khamenei alionya kuhusu siasa za makusudi zinazolenga kulisahaulisha suala la Palestina. Alisisitiza:
“Mataifa ya Kiislamu hayapaswi kuruhusu fikra za umma zielekezwe mbali na Palestina, Gaza, na jinai za utawala wa Kizayuni kwa kutumia uvumi na maneno yasiyo na maana.”

Ayatollah Khamenei alisisitiza umuhimu wa kushikamana na kupinga utawala wa Kizayuni na wafuasi wake. Alisema:
Marekani inatoa msaada wa halisi kwa utawala wa Kizayuni. Ingawa katika siasa kuna maneno ambayo yanaweza kuwa na tafsiri tofauti, ukweli ni kwamba watu wa Palestina na Gaza hawakabiliani tu na utawala wa Kizayuni, bali pia na Marekani na Uingereza. Badala ya kuzuia jinai na mauaji, wanamsaidia muuaji kwa kupeleka silaha na vifaa.”

Kiongozi huyo aliongeza kwamba baadhi ya matamshi, maneno, na matukio ya muda mfupi hayapaswi kumaliza au kupunguza umuhimu wa suala la Palestina. Alisisitiza:
“Kwa neema na utukufu wa Allah, Palestina itashinda dhidi ya watawala wa Kizayuni na wingu la uongo litakwisha. Kama vile wanavyofanya huko Syria, hiyo si ishara ya nguvu yao bali ni dalili ya udhaifu na italeta udhaifu zaidi.”

Ayatollah Khamenei alielezea matumaini yake kuwa watu wa Iran na mataifa mengine yenye imani wataona ushindi wa Palestina dhidi ya wavamizi wa ardhi hiyo.

Katika mwanzo wa mkutano, Waziri wa Ushirikiano, Kazi na Ustawi wa Jamii, alisisitiza umuhimu wa kuboresha hali ya wafanyakazi na kusema:
“Kuboresha hali ya wafanyakazi ni kuboresha hali ya jamii nzima. Wafanyakazi ni nguvu inayoendesha sera za uchumi wa nchi, na ushiriki wao katika kuunda na kutekeleza sera utakuwa ufunguo wa kufungua njia ya uzalishaji na sekta ya viwanda.”

Waziri pia alitaja baadhi ya vipaumbele na mipango inayolenga kuboresha hali ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na:

  • Kufuatilia utekelezaji wa sheria na sera za kazi na uzalishaji.

  • Kupanga malengo ya kupunguza kwa asilimia 8 matukio ya ajali za kazini ifikapo mwaka 2025 - 2026.

  • Kulinda uwezo wa kununua wa wafanyakazi.

  • Kugawa vyeti vya bidhaa (calaberg).

  • Kuimarisha utamaduni wa kazi kwa kuondoa ile kati kati (middlemen).

  • Kupunguza gharama za jamii ya wafanyakazi kwa kuboresha mifumo ya elimu na afya.

  • Kufuatilia suala la makazi ya wafanyakazi.

  • Kutambua na kuenzi hadhi ya wafanyakazi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha