10 Mei 2025 - 22:04
Source: Parstoday
Duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja baina ya Iran na Marekani kuanza kesho

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidi, ambaye anakaimu nafasi ya mpatanishi kati ya Iran na Marekani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, ametangaza kuwa duru ya nne ya mazungumzo hayo itafanyika mjini Muscat kesho Jumapili.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa amesema kuhusu duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kesho Jumapili kati ya Iran na Marekani kwamba: "Tunasubiri maelezo kutoka upande wa Oman kuhusu muda wa kuanza mazungumzo."

Sayyid Abbas Araghchi alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na kuongeza kuwa: "Kuhusu wakati na mahali pa mazungumzo hayo ni suala ambalo litaamuliwa na nchi mwenyeji au mpatanishi, ambayo ni Oman. Marafiki zetu wa Oman walituuliza kuhusu Jumapili na sisi tumekubali. Inavyoonekana, wamezungumza pia na upande mwingine, na hadi sasa, mazungumzo yamepangwa kufanyika Jumapili, Mei 11. Tunasubiri maelezo kutoka upande wa Oman kuhusu wakati wa kuanza mazungumzo hayo."

Duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja baina ya Iran na Marekani kuanza kesho

Kuhusu maendeleo katika mazungumzo hayo, Araghchi alisema: "Kwa vyovyote vile, mazungumzo yanaendelea na ni jambo la kawaida kwamba kadiri tunavyosonga mbele ndivyo mashauriano na mapitio yanavyohitajika zaidi, na wajumbe wanahitaji muda zaidi wa kupitia masuala yaliyoibuliwa, lakini jambo muhimu zaidi ni kwamba tunasonga mbele."

Akisisitiza kwamba misimamo ya Iran katika mazungumzo ni ya kisheria na haiwezi kubadilika, Araghchi amesema: "Tunaenda kwenye njia iliyoainishwa kwa mujibu wa kanuni tulizoweka. Lakini tunapokea ujumbe unaogongana kutoka upande wa pili, watu tofauti wanasema mambo tofauti. Wakati mwingine, hata maneno ambayo mtu anasema yanagongana na maneno yake ya siku hiyo hiyo au siku inayofuata. Hili ni moja ya matatizo tuliyo nayo kwenye mazungumzo haya, na wengine wanaamini kuwa ni kutokana na kuanza utawala mpya huko Marekani na kwamba bado hawajatulia au hawajajipanga vizuri. Wengine wanaona kuwa ni njama za kawaida za Wamarekani."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Sisi hatushughulishwi na mambo yao, sisi tutafuata njia yetu wenyewe, na misimamo yetu iko wazi kabisa, na tutasimama kidete kulinda haki zetu."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha