16 Mei 2025 - 21:36
Source: Parstoday
Trump atoa matamshi mapya kuhusu mazungumzo na Iran

Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena leo Ijumaa ametoa matamshi mapya kuhusu mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya nchi yake na Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, rais wa Marekani Donald Trump, wakati wa ziara yake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) leo Ijumaa, amerudia tena matamshi yake yenye nyuso mbili yaani kudai anataka mazungumzo na wakati huo huo anatoa vitisho.

Amedai kuwa Marekani itasuluhisha kadhia ya Iran kwa njia yoyote iwezekanayo. Amesema: "Tutasuluhisha hali hii kwa asilimia 100. Imma kwa uzuri na kwa amani, au kwa sura isiyopendekeza."

Lakini muda wote viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa, hawakubali kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo. Taifa hili la Kiislamu liko imara pande zote na halitetereki katika kulinda haki zake.

Mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani kuhusu suala la nyuklia yalianza mwezi uliopita wakati wa muhula wa pili wa urais wa Donald Trump, kwa lengo la kushughulikia mpango wa nyuklia wa Iran na kuondoa vikwazo. Mazungumzo haya yameanza kufuatia juhudi za kidiplomasia za imma kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA au kufikia makubaliano mapya. Inachojali zaidi Iran ni kuondolewa vikwazo vya kidhulma dhidi yake na kuzidi kuihakikishia dunia kwamba mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha