Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Polisi nchini Brazil hapo jana wamepambana na waandamanaji katika mji wa Sao Paulo kumpinga Rais mpya wa nchi hiyo Michel Temer ikiwa ni siku tano baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff kuvuliwa madaraka ya uongozi wa taifa hilo la Amerika ya Kusini. Polisi walilazimika kutumia gesi ya kuwasha pamoja na magurunedi ili kuwadhibiti waandamanaji hao. Idara ya usalama wa ndani nchini humo ilidai kuwa waandamanaji hao walifanya vurugu na uharibifu katika njia ya treni zinazopita chini ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwarushia polisi mawe mara baada ya kumalizika kwa maandamano hayo. Mapema hapo jana waandamanaji hao walikutana katika eneo la Copacabana mjini Rio de Janeiro wakishinikiza kung'olewa madarakani kwa Rais Temer huku pia wakidai kuitishwa kwa uchaguzi mpya. Rousseff ambaye amekata rufaa katika mahakama ya juu nchini humo kupinga kuvuliwa madaraka ameapa kufanya upinzani mkali dhidi ya Rais Temer ambaye awali alikuwa makamu wake wa Rais.
Mwisho wa habari/ 291