Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Vyuo vya Kiislamu vya Iran, alielekeza ujumbe wake kwa Papa Leo XIV, ambaye amechaguliwa hivi karibuni kufuatia kifo cha Papa Francis. Barua hiyo inaangazia maadili ya pamoja kati ya Uislamu na Ukristo, huku ikieleza matumaini ya uhusiano wa karibu zaidi kati ya jumuiya za kidini.
Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivi: "Ninakupa pongezi kwa dhati, Mheshimiwa, kwa kuteuliwa katika wadhifa huu wa juu katika uongozi wa Kanisa Katoliki," ameandika Ayatullah Arafi. Amesema cheo cha Papa ni “jukumu kubwa na fursa adhimu ya kuendeleza juhudi tukufu katika kuimarisha utakatifu, haki ya kijamii, thamani za kifamilia, mshikamano wa kidini, na mapambano dhidi ya dhuluma na ufisadi ulimwenguni.”
Aidha, ametoa rambirambi kufuatia kifo cha Papa Francis, akimsifu kwa kujitolea kwa maisha yake katika maadili mema, amani, na ucha-Mungu.
Ayatullah Arafi amesistiza “mahusiano yenye thamani” kati ya Uislamu na Ukristo, kama vile imani kwa Mwenyezi Mungu, familia, haki, na mapambano dhidi ya dhuluma. Ameongeza kuwa: "Maadili haya ya pamoja yamekuwa msingi wa mazungumzo na ushirikiano wenye manufaa kati ya dini na mataifa."
Ameelezea matumaini yake kwamba enzi ya Papa Leo XIV itaimarisha zaidi ushirikiano huo. "Ushirikiano huu unaweza kuwa daraja la kuleta amani, mshikamano wa kijamii, na maelewano ya kitamaduni na kidini ulimwenguni. "
Ayatullah Arafi alihitimisha kwa kueleza matumaini kwamba kutaendelea kushuhudiwa mabadilishano ya kitaaluma na kiutamaduni kati vyuo vikuu vya Kiislamu vya Iran na Vatican , ili kusaidia kueneza maadili ya Mwenyezi Mungu na utu.
Papa Leo XIV, ambaye awali alikuwa Askofu Robert Francis Prevost na afisa wa Vatican aliyesimamia uteuzi wa maaskofu, alichaguliwa na Baraza la Makardinali mapema mwezi huu.
Anamrithi Papa Francis, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88 baada ya miaka zaidi ya kumi ya huduma. Francis aliheshimika sana kwa kujitolea kwake kwa masikini, kuendeleza mshikamano wa kidini, na utetezi wa mazingira.
Your Comment