28 Mei 2025 - 20:17
Source: Parstoday
Iran: Hatuna cha kujadiliana na Uingereza iwapo haitaki turutubishe urani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, hakutakuwa na msingi zaidi wa mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Uingereza ikiwa London inaitaka Tehran isitishe kabisa shughuli zake za amani za kurutubisha urani, ikifuata kibubusa msimamo wa mshirika wake wa Magharibi, Marekani.

Katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X jana Jumanne, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameeleza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu imedumisha "mashirikiano ya pande nyingi" na Uingereza na wanachama wengine wa Ulaya wa makubaliano ya nyuklia ya 2015 yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).

Muingiliano kama huo, ameandika, hadi sasa umefanyika "kwa nia njema," ingawa, "Marekani inaendelea kutoonyesha nia" katika kufanya mataifa ya Ulaya kushiriki katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Washington na Tehran.

"Hata hivyo, ikiwa msimamo wa Uingereza ni 'kuiitaka Iran irutubishe urani kwa kiwango cha sifuri…, hakuna kitu kilichobaki kwetu kujadili kuhusu suala la nyuklia," Araghchi amesisitiza.

Matamshi hayo yamekuja baada ya Peter Mandelson, Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa kusema katika hotuba yake katika Baraza la Atlantiki huko Washington, D.C kwamba "Uingereza inaunga mkono kwa dhati mpango wa Rais wa [Marekani] [Donald Trump] katika kujadili juu ya kuzuia Iran kurutubisha madini ya urani. 

Kabla ya hapo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema kwamba, taifa la Iran halitikisiki mbele ya mbinu za mashinikizo za Marekani, na kutupilia mbali madai ya Washington yanayotaka Jamhuri ya Kiislamu iachane na haki yake halali ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Esmaeil Baghaei katika mahojiano na CNN, kama ilivyoripotiwa kwenye tovuti ya kituo hicho amesema, "Wairani hawatalegezwa kwa mashinikizo yoyote." 

Your Comment

You are replying to: .
captcha