Kwa mujibu wa duru za Palestina, mwezi Mei 2025, walowezi 12,378 wa Kizayuni walivamia msikiti wa Al-Aqsa kwa visingizio mbalimbali vikiwemo vya utalii na kuungwa mkono na serikali inayoikalia kwa mabavu na vikosi vyake vya usalama.
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Palestina, mwezi uliopita, walowezi walianza kufanya ziara za uchochezi katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa na kufanya sherehe za Talmudi katika sehemu hiyo takatifu. Makundi na wafuasi wa Kizayuni walisherehekea kile kinachoitwa "Siku ya Umoja wa Quds" katika Msikiti wa Al-Aqswa katika kumbukumbu ya mwaka huu, na sherehe hizo zilihudhuriwa na marabi wakuu na mawaziri wa baraza la mawaziri la Netanyahu akiwemo Ben-Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani na Bezalel Smotrich Waziri wa Fedha wa utawala huo ghasibu.
Katika majuma ya hivi karibuni, mamia ya walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakivamia uwanja wa Msikiti wa Al-Aqswa na kucheza ngoma, na kufanya sherehe za Talmudi karibu na milango ya Msikiti wa Al-Aqsa katika eneo la kale la mji wa Quds.
Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua.
342/
Your Comment