15 Juni 2025 - 13:26
Source: Parstoday
Yahya Saree: Tumelipiga kwa makombora eneo la Jaffa sambamba na mashambulizi ya Iran

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen amesema kuwa, jana nchi yake ilifanya operesheni ya kijeshi ya mafanikio dhidi ya maeneo nyeti ya adui Mzayuni katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Jaffa, kwa kulipiga eneo hilo kwa makombora mawili.

Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema: Kikosi cha makombora cha Jeshi la Yemen kimefanya operesheni dhidi ya maeneo nyeti ya adui Israel katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Jaffa kwa kutumia makombora mawili ya balestiki ya Palestina kwa nyakati tofauti katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita.

Amesema: Aidha operesheni hizo ziliratibiwa ziende sambamba na operesheni za jeshi la Iran na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH dhidi ya adui mhalifu Israel.

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinaipelekea salamu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, taifa lake, jeshi na uongozi wake kwa sababu ya ushujaa, azma, kutotetereka na imani thabiti katika kujibu jinai za kikatili za Wazayuni na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Ameongeza kuwa: Vikosi vya Ulinzi vya Yemen sambamba na kufuatilia matukio hayo kwa kujivunia, vinasisitiza kuwa hadi pale hujuma dhidi ya watu wa Ghaza zitakapokoma na mzingiro huo kuondolewa, wataendelea kushikamana na wanamapambano wa kambi ya Muqawama huko Ghaza Palestina.

Amesema: Tunayaambia mataifa mengine ya Kiarabu na Kiislamu: Jihad ni moja ya milango ya Pepo ambayo Mwenyezi Mungu ameifungua kwa wateule wake maalumu.

Amesema: Kwa hiyo chukua hatua ya kuzuia uhalifu wa Israel dhidi ya ndugu zako huko Ghaza, kwa sababu yatakayowapata wenzako leo yatakupata na wewe kesho.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha