Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei (h.a), katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1404 Hijria Shamsiyya, alikutana na maelfu ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali. Katika hotuba yake, alitaja siku za mwanzo za mwaka huu kuwa ni siku za Imam Ali (a.s) - kilele cha uadilifu, uchamungu na msamaha.

Aliwashauri Waislamu wa Iran na wa ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla kurejea katika Nahjul Balagha ili kunufaika na mafundisho ya Imam Ali (a.s), aliyemtaja kuwa mbora wa wanadamu wote baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Pia aliwahimiza wanazuoni, wanahabari na wanaharakati wa kitamaduni kuzingatia zaidi usomaji na ufundishaji wa kitabu hiki adhimu.
Kwa kuzingatia uzito wa hali nyeti inayopitia ulimwengu wa Kiislamu, hususan wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s), Shirika la Habari la ABNA limeamua kuupa kipaumbele mwaka huu ufafanuzi wa mafundisho ya Nahjul Balagha. Katika muktadha huu, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Namazi, mwalimu wa Hawza na mtafiti wa Nahjul Balagha, amekuwa akitoa maelezo ya kielimu kupitia mfululizo wa vipindi vya video kuhusu nafasi na maarifa ya Nahjul Balagha.
Maelezo ya Khutba ya 227 – Ukaribu wa Mwenyezi Mungu kwa Marafiki Wake
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Katika kuelezea hali ya marafiki wa Mwenyezi Mungu (Awliyaa), Imam Ali (a.s) anasema katika Khutba ya 227 ya Nahjul Balagha:“Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika Wewe ndiye Mwenye kutoa faraja bora kuliko wote kwa marafiki zako.” “Na Wewe ndiye uliye karibu zaidi katika kuwasimamia na kuwatosheleza waja wanaokutegemea.”
Yaani, Mwenyezi Mungu ndiye bora na wa kwanza kabisa katika kuwafariji waja wake wema, na ndiye mwenye kuwatosheleza mahitaji yao kikamilifu.
Imam (a.s) anasema pia: “Unawaona katika siri zao, na unafahamu yaliyomo nyoyoni mwao.” “Unafahamu kiwango cha uelewa wao.”
Hii ina maana kuwa Mwenyezi Mungu anajua kila lililo ndani ya nyoyo na nafsi za waja Wake, na siri zao zote ziko wazi mbele Yake, huku mioyo yao ikiwa na shauku kubwa ya kukutana na Yeye.
Dhikri na Subira; Nguzo za Awliyaa (Mawalii) wa Mwenyezi Mungu
Imam Ali (a.s) anaendelea kusema: “Iwapo upweke utawatisha, basi kukukumbuka Wewe huwaletea faraja.” “Na iwapo misiba itawashukia kwa wingi, basi hukimbilia kwako kwa kutafuta hifadhi.”
Kwa nini hivyo? Kwa sababu wanajua kwamba: “Hatima ya mambo yote iko mikononi Mwako, na kila jambo hutokana na maamuzi Yako.”
Kwa ufahamu huo, wanamtegemea Mwenyezi Mungu kikamilifu, wanampenda kwa dhati na wanashikamana Naye katika kila hali.

Dua ya Mwisho ya Imam Ali (a.s): Mwongozo na Msamaha wa Mwenyezi Mungu
Katika hitimisho la khutba hiyo, Imam Ali (a.s) anamuomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Ewe Mola wangu! Ikiwa sitajua nini kukuomba, au nikipofuka nisijue nini kinanifaa, basi niongoze mwenyewe kwenye yaliyo na kheri kwangu.” “Ichukue moyo wangu na uniongoze katika njia ya uongofu.” “Haya siyo mambo mageni katika uongofu Wako, wala si mbali na ukarimu Wako wa kunisitiri.”
Kisha anaomba kwa unyenyekevu mkubwa: “Ewe Mola wangu! Nitendee kwa msamaha Wako, wala usinitendee kwa uadilifu Wako.”
Kwa sababu, lau uadilifu wa Mwenyezi Mungu ungekuwa ndio kipimo pekee, basi hakuna mwanadamu ambaye angenusurika. Ndiyo maana Ahlul-Bayt (a.s) wanatufundisha daima kukimbilia katika rehema, msamaha na fadhila za Mwenyezi Mungu.
Na Amani iwe juu yenu, na Rehema na Baraka za Mwenyezi Mungu
Your Comment