Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Abu Dhabi – Falme za Kiarabu (UAE) | Mwanamfalme wa Saudi Arabia na Mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi wa nchi hiyo, Turki Al-Faisal, amesema kuwa tishio kubwa linaloikabili Mashariki ya Kati kwa sasa si Iran, bali ni utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akizungumza katika mkutano maalumu uliofanyika mjini Abu Dhabi, Turki Al-Faisal amesisitiza kuwa Israel ndiyo chanzo kikuu cha misukosuko na migogoro ya mara kwa mara katika ukanda huo, na kwamba juhudi za kurejesha amani na utulivu haziwezi kufanikiwa bila Marekani kuichukulia kwa uzito Israel na kuiwajibisha kwa vitendo vyake.
Amesema: “Israel inaendelea kusababisha matatizo katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Ikiwa Marekani kweli inataka kuona amani na utulivu ukirejea, basi haina budi kuidhibiti Israel na kuizuia kuendelea na mashambulizi yake ya kiholela.”
Mashambulizi Dhidi ya Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon na Syria Yakemewa
Turki Al-Faisal amekosoa vikali mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya maeneo mbalimbali ikiwemo Ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon na Syria, akisema mashambulizi hayo yanaonyesha wazi kuwa Israel inajihisi ipo juu ya sheria za kimataifa na haina mpinzani wa kuzuia uchokozi wake.
Kwa mujibu wake, hali hiyo imeifanya Israel iendelee kutenda uhalifu wa kivita bila kuogopa adhabu wala lawama kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Shambulizi Dhidi ya Ujumbe wa Hamas Qatar ni Onyo kwa Nchi za Ghuba
Katika kauli yake nzito, Turki Al-Faisal pia amebainisha kuwa shambulizi la Israel dhidi ya ujumbe wa Hamas nchini Qatar lilikuwa ujumbe wa vitisho kwa nchi za Ghuba, akisema hatua hiyo ilikuwa onyo la wazi kuwa mataifa ya Ghuba yako katika hatari na yanapaswa kuchukua tahadhari za pamoja za kiulinzi.
Amesema tukio hilo linapaswa kufungua macho ya nchi za Ghuba kuwa Israel haitambui mipaka ya sheria wala heshima ya mamlaka za mataifa mengine.
Msimamo Wake Waunga Mkono Mpango wa Ulinzi wa Pamoja wa Nchi za GCC
Matamshi ya Turki Al-Faisal yanakuja katika kipindi ambacho nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) zinaendelea kujadili na kupanga mfumo wa pamoja wa ulinzi wa anga, unaolenga kukabiliana na vitisho vya kijeshi vinavyozidi kuongezeka katika eneo hilo, vikiwemo vile vinavyotoka upande wa Israel.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kauli ya Turki Al-Faisal ina uzito mkubwa, kutokana na nafasi yake ya zamani katika ujasusi na uzoefu wake mpana wa masuala ya usalama wa kikanda.
Your Comment