9 Desemba 2025 - 14:49
UMOJA WA MATAIFA: Nusu ya Wakazi wa Afghanistan Wanahitaji Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa mwaka 2026 takribani watu milioni 22 — sawa na asilimia 45 ya watu wa Afghanistan — watahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu; huku idadi ya watu wenye uhaba mkali wa chakula ikifikia milioni 17.4 na milioni 5.2 wakiwa katika hatari ya njaa kali.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika ripoti yake mpya imesema kuwa mwaka 2026 karibu nusu ya watu wa Afghanistan (milioni 21.9, sawa na asilimia 45 ya idadi ya watu) watakuwa wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.

OCHA imesema kuwa ingawa idadi hii imepungua kwa asilimia 4 ukilinganisha na mwaka 2025, bado Afghanistan inabaki kuwa miongoni mwa maeneo yenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani katika mazingira yasiyo ya vita wazi.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa uhaba wa chakula nchini Afghanistan umefikia hatua ya hatari na imeongeza kuwa inakadiriwa watu milioni 17.4 watakabiliwa na njaa kali mwaka ujao, ambapo milioni 5.2 kati yao watakuwa katika kiwango cha "dharura" (Hatua ya 4) — idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ya mwaka uliopita.

Taasisi hiyo ya kimataifa imeongeza kuwa ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuathiri nchi hiyo, na kwamba mikoa 12 imeathirika vibaya huku watu milioni 3.4 wakiwa tayari wamepata madhara.

OCHA imebainisha pia kuwa kunyimwa haki kwa wanawake na wasichana kumekithiri, na kwamba vikwazo vipya vya Taliban vikijumuisha ukatili wa kijinsia, ndoa za kulazimisha za watoto na ajira za kulazimisha kwa watoto, vimefanya hatari za ulinzi kufikia kiwango cha kutisha.

Aidha, ofisi hiyo imeeleza kuwa wastani wa watu 50 hufa au kujeruhiwa kila mwezi kutokana na milipuko ya mabomu na mabaki ya vilipuzi vya kivita.

Umoja wa Mataifa umeongeza kuwa kurejea kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa Afghanistan kumeongeza mzigo mkubwa kwa serikali, ambapo umethibitisha kuwa katika mwaka 2025 zaidi ya watu milioni 2.52 wamerejea kutoka Iran na Pakistan, hali iliyosababisha changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za msingi, makazi na ajira.

Kwa mwaka 2026, Umoja wa Mataifa umeomba dola bilioni 1.72 za msaada na kusema kuwa watu milioni 17.5 (asilimia 80 ya wahitaji) watapewa kipaumbele.

OCHA imeeleza kuwa mahitaji muhimu ya Afghanistan yatakayolengwa ni pamoja na: Chakula, makazi, huduma za matibabu, maji safi ya kunywa na msaada wa fedha taslimu, huku maeneo yaliyoathiriwa zaidi yakipewa nafasi ya juu.

Mwisho wa ripoti hiyo umeonya kuwa endapo msaada wa kimataifa hautotolewa kwa wakati, hatari ya vifo vinavyotokana na njaa na magonjwa miongoni mwa watoto, wanawake na wazee itaongezeka kwa kiwango kikubwa.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha