Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- jana, soko la Tehran lilikumbwa na mkusanyiko wa maandamano ya baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa sekta ya biashara kufuatia kuyumba kwa kiwango kikubwa kwa thamani ya fedha za kigeni.
Mkusanyiko huu, uliotokana na kupanda kwa bei kupita kiasi na kupungua kwa uwezo wa ununuzi wa wananchi, uliakisi wasiwasi mkubwa wa wafanyabiashara na wanaharakati wa kiuchumi kuhusu hali ya sasa ya soko na uchumi wa nchi.
Washiriki wa soko wakati wa mkusanyiko wa jana na pia mikusanyiko kadhaa ya leo waliitaka serikali ichukue hatua za kusaidia kuleta uthabiti katika kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni, pamoja na kutoa motisha za kikodi na mikopo ya uwekezaji.
Wakati waandamanaji walipokuwa wakieleza madai yao ya haki, baadhi ya vyombo vya habari pinzani vya Kifarsi vilijikita katika kuripoti matukio yenye kuvunja maadili kwa namna mbalimbali, kwa lengo la kuchochea taharuki na kuyasogeza pembeni madai halisi ya wananchi.
Inaonekana wazi kuwa baadhi ya vyombo hivi, kwa kukataa kuzingatia madai ya msingi ya wafanyabiashara, vinajaribu kuchochea migogoro na misukosuko ya kijamii.
Aidha, baadhi ya mitandao na makundi yenye historia ya kuchochea machafuko katika matukio ya awali, yaliendelea na juhudi zao za kutoa wito wa mikusanyiko mipya. Vyombo vya habari vinavyopinga Iran na matawi yake katika mitandao ya kijamii, jana na leo, vilitumia mbinu na hila mbalimbali za kihabari ili kuelekeza madai ya wananchi kwenye mwelekeo wanaoutaka wao.
Ripoti na ushuhuda wa moja kwa moja wa leo Jumanne, tarehe 30 Desemba, 2025 unaonesha kuwa mwitikio wa umma kwa wito huo ulikuwa hasi, na wananchi walichagua kudumisha utulivu na uthabiti katika jamii. Juhudi za kambi pinzani, isipokuwa harakati chache sana, hazikufua dafu.
Mikusanyiko ya jana katika soko la Tehran, ambayo ilitumiwa sana na vyombo vya habari vya Kizayuni na Magharibi, leo ilishuhudia hali ya utulivu mkubwa, na wito wa vyombo vya habari pinzani wa kufanya mkusanyiko leo haukupata mwitikio wa wananchi.
Wakati huo huo, mikusanyiko midogo iliundwa katika baadhi ya vyuo vikuu vya Tehran, ikiwemo Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif na Chuo Kikuu cha Tehran, ambapo idadi ya washiriki ilibaki kuwa mamia machache. Hata hivyo, mikusanyiko hiyo ilimalizika haraka bila kupanuka wala kuleta mabadiliko katika hali ya jumla, kutokana na kukosa uungwaji mkono mpana wa wanafunzi.
Katika muktadha huo, vyombo vya habari kama BBC Persian, pamoja na kuripoti kwa kina mkusanyiko wa jana na harakati za watu wanaotiliwa shaka, kwa wakati huo huo vilidai kuwa “hafla ya tarehe 9 Dey jijini Tehran haikufanyika”, na kudai kuwa hafla hiyo ya kuadhimisha siku ya kihistoria ya 9 Dey “ilifanyika katika majimbo matatu pekee.”
Hali hii ni kinyume na tangazo rasmi lililotolewa siku zilizopita, lililobainisha kuwa hafla za 30 Desemba zingefanyika katika majimbo yote ya nchi, huku hafla kuu na maalum ikipangwa kufanyika Tehran. Hafla ya kuadhimisha Siku ya Mwenyezi Mungu ya 9 Dey ilifanyika leo alasiri katika Uwanja wa Imam Hussein (a.s) jijini Tehran kwa ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi, na kwa hotuba ya Hujjatul-Islam Hajji-Sadeghi, mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na ilirushwa mubashara.
Mbali na Tehran, katika majimbo mengine pia hafla za kuadhimisha Siku ya Mwenyezi Mungu ya 9 Dey zilifanyika kwa ushiriki wa wananchi na kwa kulaani fitna za mwaka 1388, na picha zake zilisambazwa katika vyombo mbalimbali vya habari. Hata hivyo, BBC Persian, kwa makusudi na kama ilivyo desturi yake, ilipuuza matukio haya muhimu.
Kwa kuzingatia hali ya sasa na umuhimu wa kushughulikia madai ya haki ya wafanyabiashara, inaonekana kwamba endapo kuyumba kwa thamani ya fedha na matatizo ya kiuchumi hayatatatuliwa, uwezekano wa kuendelea kwa aina hizi za maandamano upo. Hata hivyo, juhudi za wapinzani za kuchochea machafuko zinaonekana kuwa hazina matokeo.
Pamoja na hayo, kuna haja kwa viongozi kuzingatia kwa dhati madai ya kiuchumi na kijamii ya wananchi na kuchukua hatua za msingi zaidi za kuleta uthabiti na utulivu katika jamii; hatua ambazo zinaweza kuzuia kuongezeka kwa hali ya kutoridhika na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi.
Your Comment