31 Desemba 2025 - 23:44
Theluthi moja ya Waisraeli wanahitaji msaada wa kitaalamu wa kisaikolojia

Matokeo ya utafiti mpya yanaonyesha kuwa takriban theluthi moja ya Waisraeli wanahitaji msaada wa kitaalamu wa kisaikolojia, huku athari za vita vya Gaza kwa zaidi ya miaka miwili sasa zikiendelea kuliweka jamii ya Israel chini ya shinikizo kubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, matokeo ya utafiti wa maoni uliotolewa leo Jumatano yanaonyesha kuwa migogoro ya kisaikolojia katika jamii ya Israel imeongezeka kwa kiwango kikubwa kadiri mwaka 2025 unavyokaribia kuisha. Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 32 ya Waisraeli kwa sasa wanahitaji msaada wa kitaalamu wa kisaikolojia, kutokana na athari za vita vinavyoendelea Gaza kwa zaidi ya miaka miwili.

Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Times of Israel, utafiti huo ulifanywa Novemba iliyopita na Huduma za Afya za Maccabi, mojawapo ya taasisi kubwa zaidi za afya nchini Israel. Utafiti huo ulihusisha sampuli wakilishi ya watu 1,100, wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 75, kutoka maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Matokeo yanaonyesha kuwa asilimia ya watu wanaohitaji msaada wa kisaikolojia imefikia kiwango kisichokuwa cha kawaida, na imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya kabla ya vita, jambo linalodhihirisha kina cha athari za kisaikolojia na kijamii za vita hivyo.

Aidha, asilimia 17 ya washiriki walisema hali yao ya kisaikolojia ni ya wastani au duni, ilhali kabla ya kuanza kwa vita vya Gaza, ni asilimia 13 tu waliokuwa katika hali hiyo.

Wanajeshi wameathirika zaidi

Utafiti huo unaonyesha kuwa hali ya kisaikolojia ya wanajeshi waliotumikia katika mwaka uliopita ni mbaya zaidi, ambapo asilimia 39 walisema wanahitaji msaada wa kisaikolojia, asilimia 26 wana wasiwasi kuhusu unyogovu, na asilimia 48 wanakabiliwa na matatizo ya usingizi.

Matokeo haya yanakuja sambamba na tamko la jeshi la Israel siku ya Jumanne, lililosema kuwa visa 21 vya kujiua miongoni mwa wanajeshi vimesajiliwa tangu mwanzo wa mwaka 2025, huku shinikizo la kisaikolojia linalotokana na kuendelea kwa vita likizidi.

Takwimu zinaonyesha pia kuwa mgogoro wa kisaikolojia miongoni mwa Waisraeli umezaa athari nyingine, ikiwemo ongezeko la matumizi ya tumbaku, ambapo asilimia 30 ya watumiaji wa bidhaa za tumbaku walisema wameongeza matumizi yao mwaka 2025 kutokana na msongo wa mawazo na shinikizo la kisaikolojia.

Vilevile, rekodi za afya nchini Israel zinaonyesha kupungua kwa idadi ya vizazi kwa asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka 2024, jambo linaloashiria athari za vita katika maamuzi ya kifamilia na uthabiti wa kijamii.

Takwimu hizi zinachapishwa wakati ambapo Israel inaendelea na vita dhidi ya Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023, vita ambavyo hadi sasa vimesababisha zaidi ya mashahidi 71,000 na majeruhi 171,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, huku jamii ya kimataifa ikiituhumu Israel kwa kutekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha