19 Machi 2011 - 20:30

Kwa mtazamo wa weledi wa mambo na wanaharakati wa kisiasa nchini Libya utungaji wa katiba, kukusanya silaha zilizoko mikononi mwa watu, kuunda serikali, kuondoka vikosi vya kijeshi vya NATO na kuzikomboa mali za umma zinazoshikiliwa na nchi za Magharibi ndizo changamoto muhimu zaidi zinazoikabili Libya baada ya kifo cha Muammar Gaddafi

Kwa mtazamo wa weledi wengi wa siasa za Libya mwisho wa uhai wa Gaddafi ndio mwanzo wa changamoto kubwa zitakazoikabili Libya. Alhadi Shaluf, kiongozi wa chama cha Uadilifu na Demokrasia cha Libya amesema kutungwa katiba mpya ni miongoni mwa changamoto muhimu zaidi inayopasa kushughulikiwa nchini humo.Idris Adbish, mwanaharakti wa kisiasa wa Libya, yeye anaitakidi kuwa kukusanywa silaha zilizoko mikononi mwa raia ndio changamoto ya kiusalama inayoikabili Libya ya baada ya Gaddafi. Amma Muhammad Mahmoud ash Sharkasi ambaye ni mtaalamu na mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Benghazi yeye anaamini kwamba kuundwa serikali mpya ni moja ya changamoto muhimu inayoikabili Libya mpya. Sambamba na kuashiria nukta kwamba kwa muda wa miaka 40 wananchi wa Libya wametengwa katika masuala ya uendeshaji nchi na kuburuzwa na kutwishwa kila jambo, mhadhiri huyo wa taaluma ya siasa amesisitiza kuwa kuundwa serikali nchini Libya kunahitajia akili, busara, uelewa na ushirikishaji wa watu wa matabaka yote ya nchi hiyo. Alaa bin Dardaf ambaye ni mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa yeye anaitakidi kuwa kuachiliwa mali za Libya zinazoshikiliwa na nchi za Magharibi ni changamoto muhimu ambayo nchi hizo zinaweza kuitumia ili kuwa na ushawishi na kuingilia masuala ya ndani ya Tripoli. Alaa bin Dardaf ameongeza kuwa nchi za Magharibi hazina kisingizio tena cha kuzizuia mali za Libya kwa kuwa kitambo sasa mafuta ya Libya yamekuwa yakizalishwa na kuuuzwa kwenye masoko ya nchi hizo, hivyo inapasa mali zote za Libya zinazoshikiliwa zikabidhiwe kwa serikali ya nchi hiyo. Amma Abayomi Azikiwe ambaye ni mhariri wa mtandao wa habari wa Pan-African anasema suala muhimu zaidi kwa sasa ni kuondoka kwanza vikosi vya kijeshi vya NATO katika ardhi ya Libya. Hata hivyo kwa mtazamo wa Azikiwe ni jambo lililoko mbali kuwa Marekani na NATO zitakuwa tayari kuondoka huko na kuwapa fursa wananchi wa Libya ya kufanya kazi ya kuijenga upya nchi yao