19 Machi 2011 - 20:30

Utamaduni na sanaa ya Kiislamu vinachunguzwa katika kikao kinachofanyika leo katika Chuo Kikuu cha Texas katika mji wa Arlington. Kila muhula wa masomo Kundi la Sanaa na Historia la chuo hicho hushirikiana na Baraza la Kiislamu la Agha Khan la Texas Kaskazini katika kuandaa vikao vinavyojadili masuala mbalimbali yanayohusiana na Uislamu ambapo katika muhula huu nembo zilizokuwa zikitumiwa na wafalme wa Kiislamu katika zama za kale zitachunguzwa.

Ripoti ya ABNAKatika kikao hicho Machael Berry, mhadhiri wa masuala ya Asia ya Karibu (Asia Minor) katika Chuo Kikuu cha Princeton atatoa hotuba kuhusiana na sanaa ya picha, filamu, michoro na nembo za kifalme katika sanaa na utamaduni wa Kiislamu.

Mhadhiri huyo amesema kuwa atajaribu kuonyesha katika kikao hicho uhusiano mkubwa wa kisanii na kiutamaduni uliopo kati ya Waislamu, Wakristo na Mayahudi.

Wahadhiri wengine waliopangiwa kuzungumza katika kikao hicho wamesema kuwa kikao hicho kina umuhimu mkubwa kwa sababu kitawafahamisha Wamarekani kwamba utamaduni wa Ulaya na nchi za Kiislamu umekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha utamaduni wa wanadamu na kwamba kuna mambo mengi yanayofanana katika utamaduni wa Magharibi na wa nchi za Kiislamu. Wamesema kwamba kikao hicho kitasaidia pakubwa kurekebisha mtazamo mbaya unaoonekana katika nchi za Magharibi kuhusiana na ulimwengu wa Kiislamu.

Wahadhiri hao wameongeza kuwa kikao hicho pia kitajaribu kujenga uhusiano wa kidini kati ya makundi mbalimbali ya kiutamaduni na kutoa mtazamo mmoja wa kimataifa kuhusiana na suala la sanaa na utamaduni.