10 Novemba 2014 - 16:03
Marais wakutana katika mkutano wa  wa APEC

Viongozi wa China na Japan wamefanya mkutano wa nadra baina yao hii leo baada ya miaka miwili ya uhasama kati ya nchi zao. Mazungumzo yao yanafanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele wa nchi za Asia na Pacifiki APEC.

Viongozi wa China na Japan wamefanya mkutano wa nadra baina yao hii leo baada ya miaka miwili ya uhasama kati ya nchi zao. Mazungumzo yao yanafanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele wa nchi za Asia na Pacifiki APEC.
Rais wa China Xi Jinping na Waziri mkuu wa Japan wamekutana katika kile ambacho Abe amekitaja kuwa hatua ya kwanza katika kurekebisha uhusiano uliovunjika kati ya nchi hizo mbili zenye nguvu za kiuchumi.
China ambayo ni ya pili kwa uchumi imara duniani, na Japan ambayo iko katika nafasi ya tatu, zimekuwa zikizozana vikali kwa miaka miwili iliyopita kuhusu visiwa, utawala wa eneo na tatizo la muda mrefu kuhusu vita kati ya nchi hizo mbili ambapo majeshi ya Japan yaliivamia China kufanya mauaji na kuitawala.
Rais wa Marekani Barrack Obama naye amewasili nchini China hii leo kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano wa nchi za Asia na Pacific APEC ambao pia unahudhuriwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye nchi yake na Marekani zimeshuhudia uhusama baridi katika miezi ya hivi karibuni.
Obama ambaye yuko katika ziara ya siku nane barani Asia na Pacific amesema anaona kasi ikizidi katika kuafikiwa kwa makubaliano ya kuwepo biashara huru ya mpango unaopendekezwa na nchi yake utakaozihusisha nchi 12 tu kati ya nchi wanachama 21 wa APEC ujulikanao TPP.
Yafaa kuashiria kuwa,Mkutano huo wa APEC ndiyo mkubwa kabisa kuwahi kuandaliwa na rais wa China tangu achukue madaraka mwaka jana na unawaleta pamoja viongozi wa baadhi ya nchi kubwa kiuchumi duniani kwa siku mbili zijazo wakiwa na lengo la kuboresha uhusiano wa kibiashara kati yao na pembezoni mwa mkutano huo wakijaribu kushughulikia masuala ya siasa za udhibiti wa kanda.
China na Marekani zinatarajiwa kila mmoja kusukuma ajenda tofauti za kufikiwa kwa makubaliano ya kibiashara ambayo hayahusishi upande mwingine.Mkutano wa APEC utapiga darubini ushindani uliopo kati ya nchi kubwa zilizostawi kiuchumi Marekani, China na Urusi.
Putin na Xi walikutana hapo jana ambapo kiongozi wa China alimuambia Putin kuwa aendelee kuvuna matunda ya urafiki wao. Xi alimuambia Putin kuwa licha ya mambo katika ulingo wa kimataifa kuonekana kubadilika wanapaswa kusalia katika njia waliyoichagua ya kutanua na kuimarisha ushirikiano mzuri kati yao.
Mkutano huo wa APEC unafungua wiki ya mikutano mingine ya ngazi ya juu ambapo baada ya Beijing, viongozi wanatarajiwa kuelekea Myanmar kwa mkutano wa kilele wa kiuchumi wa nchi za mashariki mwa Asia na kufuatiwa na mazungumzo ya nchi ishirini zenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani G20 utakaofanyika mjini Brisbane,Australia.

Tags