Jeshi la Israel leo limewatanya takribani waandamanaji 300 wa Kipalestina waliokuwa wakirusha mawe katika mji wa Hebron ulioko katika Ukingo wa Magharibi. Makabiliano hayo ya leo ni muendelezo wa uhasama ambao umezidi kupamba moto katika siku za hivi karibuni kati ya Israel na Palestina kuhusiana na madai kuwa Israel ina mipango ya kubadilisha makubaliano kuhusu haki ya kuabudu kwa Waislamu katika eneo takatifu mashariki mwa Jerusalem ambako kuna msikiti wa al-Aqsa, madai ambayo waziri mkuu wa Israel ameyakanusha. Kwa wiki ya pili mfululizo, Israel imewaruhusu Waislamu wa kila umri kusali katika msikiti huo. Kiasi cha waislamu 45,000 wamehudhuria sala ya leo ya Ijumaa. Wakati huo huo, Israel imelitupilia mbali pendekezo la nchi tano wanachama wa Umoja wa Ulaya kutozibomoa nyumba za washambuliaji wa Kipalestina waliofanya mashambulizi mjini Jerusalem,ikisema hatua hiyo ni kuwazuia wengine kufanya hivyo siku za usoni.