Serikali ya Urusi imepeleka meli za kivita karibu na nchi za Ufaransa na Uingereza.
Maafisa wa serikali ya Ufaransa na wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamethibitisha kuwepo kwa meli nne za kivita katika bahari inayoziunganisha Ufaransa na Uingereza, lakini wamekataa kuthibitisha ikiwa meli hizo zilikuwepo kwa mazoezi ya kijeshi au kukimbia hali mbaya ya hewa. Msemaji wa jeshi la majini la Ufaransa amesema si jambo la ajabu kwa meli hizo kuwapo hapo, huku msemaji wa NATO akisema meli hizo hazikuwa zikifanya mazoezi, kama ambavyo vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti hivi leo. Mapema ripoti za vyombo vya habari zilikuwa zinaashiria kuwa Urusi imetuma meli zake kwenye bahari hiyo. Urusi na mataifa ya Magharibi zina mgogoro mkubwa juu ya dhima ya Urusi kwenye eneo la mashariki mwa Ukraine, ambapo mataifa ya magharibi yanaishutumu Urusi kwa kuingiza majeshi yake Ukrane na kusababisha hali ya amani kuwa tete nchini humo.
Uwepo wa meli hizo katika maeneo hayo umesababisha mshtuko mkubwa kwa Ufaransa, kwani serikali ya Urusi ilitoa onyo kali kwa Ufaransa baada ya kuzuia meli za kivita za nchi hiyo.