1 Desemba 2014 - 18:18
Maandamano yazuia majaji kufika mahakamani Misri

Maandamano makali ya kupinga hukumu ya mahakama iliyomtoa hatia ya mauaji Dikteta Hosni Mubarak yamepelekea majaji kushindwa kufika mahakamani.

   Maandamano makali ya kupinga hukumu ya mahakama iliyomtoa hatia ya mauaji Dikteta Hosni Mubarak yamepelekea majaji kushindwa kufika mahakamani.

 Mahakama iliyotazamiwa kuwahukumu kifo takribani wafuasi 500 wa upinzani nchini Misri imeshindwa kukutana, siku mbili tu baada ya kumfutia hatia za mauaji na ufisadi rais wa zamani, Hosni Mubarak.

Leo ilitazamiwa kuwa siku nyengine ya hukumu za mpigo za kifo zinazotolewa na mahakama za Misri dhidi ya wafuasi wa upinzani lakini majaji walishindwa kufika na washukiwa hawakuweza kuingia kwenye ukumbi wa mahakama iliyojaa waungaji mkono wa serikali waliokuwa wameziba nyuso zao katika chumba cha muda cha mahakama katika gereza la Tora.

   Mtandao wa Aletho News umemnukuu mkuu wa taasisi ya Reprieve ambayo inapingana na hukumu ya kifo nchini Misri, akisema: "Ghasia kwenye kesi ya leo zinaonesha uhalisia wa kesi hii kuwa ni maonyesho tu. Washukiwa na familia zao walizuia kuingia chumba cha mahakama, lakini wafuasi wa serikali wameruhusiwa kuingia wakiwa wameziba nyuso zao. Wakati huo huo, washukiwa hawa washakaa jela kwa miezi 18 na wanaambiwa watakabiliwa na kifo wakati wowote, lakini majaji hawakuhudhuria."

  Kundi hilo la washukiwa 494 lilikamatwa mwezi Agosti mwaka jana katika msako mkubwa wa vyombo vya usalama dhidi ya maandamano yanayopinga serikali, miongoni mwao wakiwa watoto wadogo wanaoshitakiwa kinyume na Sheria ya Watoto ya Misri.

   Mmoja wa watoto hao ni Ibrahim Halawa, raia wa Ireland mwenye asili ya Misri na ambaye wakati alipokamatwa alikuwa na miaka 17. Vyombo vya habari vimekuwa vikiripotiwa kuwa mvulana huyo na wenzake kadhaa wamekuwa wakiteswa na kuzuiwa kupata matibabu.

Kama kwa wenzao wengine, washukiwa hawa 494 nao wanatazamiwa kuhukumiwa kifo, hukumu ambazo zimezuwa lawama kali kutoka Umoja wa Mataifa, Marekani na makundi ya kutetea haki za binaadamu ndani ya Misri kwenyewe.

   Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, mahakama ya mji wa kusini mwa Misri wa Minya, iliwahukumu kifo watu 638 kwa mpigo. Hukumu hiyo ilitanguliwa na ile ya mwezi Machi, ambapo wengine 529 walipewa hukumu kama hiyo, ikisadifiana na ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya nje wa Misri nchini Marekani, ambapo serikali ya Rais Barack Obama ilisema hukumu hizo "zinakiuka misingi ya kimataifa ya haki."

Katika hukumu nyengine ya jumla jamala hivi karibuni, mahakama ilitoa adhabu ya kifungo cha miaka 378 kwa watoto 78, ambapo mawakili wao walizuiwa kuhudhuria.

   Wakati hayo yakiendelea, sehemu kadhaa nchini Misri zimeendelea kushuhudia maandamano ya umma kwa siku ya pili mfululizo, kufuatia uamuzi wa mahakama kuu hapo Jumamosi kumfutia hatia za mauaji na ufisadi rais wa zamani, Hosni Mubarak, wanawe na maafisa kadhaa wa utawala wake.

Wanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Al-Azhar, pia kwenye miji wa Alexandria na Ismailiya wameingai mitaani licha ya kuandamwa vikali na vyombo vya usalama. Watu wawili wameshapoteza maisha hadi sasa kwenye ghasia hizo.

Hata hivyo, uamuzi wa hapo Jumamosi wa Mahakama Kuu umesifiwa na Rais Abdel-Fattah al-Sisi, ambaye kama Mubarak, ni mwanajeshi aliyejiugeuza kuwa mtawala wa kiraia, akisema sasa kamwe Misri haitarejea tena kwenye zama za giza.

Yafaa kuashiria kwamba Dikteta Hosni Mubaraka ameachiwa huru kwa tuhuma ya kuua waandamanaji waliopelekea kutolewa kwake madarakani, kwa upande mwingine wapinzani walioshiriki kwenye maandamano dhidi ya utawala wa Jeneral Abdel-Fattah al-Sisi wanahukumiwa kifo kwa makosa ya kuchochea vurugu na kuhatarisha usalama wa nchi.

Tags