Ndege ya mizigo iliyosheheni silaha za kivita imekamatwa katika uwanja wa ndege wa Kano nchini Nigeria.
Pamoja na kuwa Urusi ilikanusha madai hayo, hatimaye serikali ya Urusi imesema inamiliki ndege ya mizigo iliyozuiwa katika uwanja wa ndege wa Kano kaskazini mwa Nigeria baada ya kugunduliwa imebeba silaha ambazo hazikuwa zimearifiwa.
Hata hivyo, Msemaji wa Ubalozi wa Urusi nchini Nigeria, ambaye aliliambia Shirika la Habari la Urusi TASS kwamba wanamiliki ndege hiyo, amesema silaha hizo ni za kikosi cha kulinda amani cha Ufaransa.
Awali, msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya kati aliiambia BBC kwamba hawafahamu chochote kuhusu helikopta mbili, magari ya kijeshi na silaha nyingine zilizokuwa katika ndege hiyo.
Masemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Ufaransa katika jamhuri ya afrika ya kati amesema kuwa wanaitambua ndege hiyo na kwamba hizo ni silaha kwa ajili ya wanajeshi wa kulinda amani walioko katika kambi ya N’damena, ambazo zitapelekwa baadaye Ufaransa.
Msemaji wa Ubalozi wa Urusi mjini Abuja alisisitiza kwa sema kuwa ndege hiyo ni yao na imebeba mzigo wa silaha kwa ajili ya walinzi wa amani.
Serikali ya Nigeria mpaka sasa haijasema kitu na imesema bado inaendelea na uchunguzi kuhusu madai hayo.
Nigeria imewekewa vikwazo vya silaha kutoka Marekani na nchi hiyo imekuwa ikiarifiwa kutumia njia zisizo halali kupata silaha kwa ajili ya kupambana na wapiganaji wa Boko haram.
Yafaa kuashiria kuwa nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa zikihusika na utumaji wa silaha kiholela kwa asasi zisizokuwa za kijeshi, jambo ambalo linaonekana kama kuchochea vita na machafuko katika nchi nyingine.