16 Machi 2025 - 14:34
Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s) anazo fadhila nyingi na daraja ya juu

Tunayo mengi ya kujifunza kutoka ndani ya Qur’an Tukufu na kutoka kwa Itrah wa Mtume, Ahlul-Bayt wake Watoharifu (amani iwe juu yao), ambavyo ndio vizito vyetu viwili na viongozi wetu baada ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w). Na kumsoma na kumzungumzia Imam Hassan Al-Mujtaba (s.a), na kujifunza mengi kutoka kwake juu ya Uislamu wetu na Maisha yetu, ni sehemu ya kushikamana kisawa sawa na Ahlul-Bayt (a.s), ambao ndio kizito cha pili kwa ukubwa baada ya Qur’an Tukufu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA -: Sheikh Rajab Shaaban, Mtafiti na mchambuzi wa masuala ya kidini, amesema kuhusiana na tukio la Mnasaba wa kuzaliwa kwa Imam Hassan (a.s) kuwa hivi sasa tupo katika masiku ambayo, historia inatueleza kwamba alizaliwa ndani yake mmoja wa watu Watukufu,waliokuwa bora kabisa katika ulimwengu huu, ambaye ni Mjukuu wa kwanza wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w), na ni Mtoto wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) na Sayyidat Fatima bint Muhammad (s.a), naye si mwingine bali ni Imam Hassan al-Mutjaba bin Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yao).

Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s) anazo fadhila nyingi na daraja ya juu

Ndugu zangu Waislamu, katika masiku haya matukufu, ambayo anazaliwa ndani yake Mtukufu huyu wa Kizazi Kitukufu cha Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), si vibaya tukawa na vikao kadhaa vya kuwazungumzia watukufu kama hawa na kutizama ni fadhila zipi wanazopambika nazo, na ni yepi mazuri tunayoweza kujifunza kutoka kwao.Na hii ni kwa sababu ya ile kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapotwambia katika sura ya pili:

۞ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na Watoto wa Ibhrahim na Watoto wa Aali Imran juu ya walimwengu wote” (Surat Aali Imran: Aya ya 33).

Kwa mujibu wa Aya hii, Mwezi Mungu alimchagua na kumuinua juu kidaraja Nabii Adam (a.s) kuliko watu wengine, lakini hili sio mahsusi kwa Nabii Adab tu pekee (a.s), bali pia alimuinua Nabii Nuh (a.s), na sio Nuh tu (a.s), bali pia na Watoto wa Nabii Ibrahim (a.s), na kisha Kizazi cha Imran (a.s). Wote hao Allah (s.w.t) amewachagua na kuwaweka juu ya walimwengu wote kidaraja.

Na hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu anapowanyanyua Daraja watukufu hawa, anataka wawe ni kiigizo chema kwetu katika matendo yetu tunayoyatenda katika dunia hii. Na unapotizama Kizazi cha Nabii Ibrahim (a.s), huwezi kumkosa ndani yake Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s).

Hivyo, nukta ya msingi kuizingatia katika Aya hii Tukufu kuhusu watu hawa Watukufu ambao Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kuwa amewachagua na kuwanyanyua daraja juu ya walimwengu wote, ni hii kuwa: Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewachagua na kuwaweka ili wawe kiigizo chema kwetu, na tujifunze kutoka kwao katika yale waliyoyatenda na kuyafundisha katika dunia hii, ili tuweze kuifikia ile daraja ya kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu.

Imam Hassan al-Mutjaba (a.s) ana sehemu nyingi za fadhila ambazo unaweza kumzungumzia. Kabla ya kutizama fadhila zake ni zipi, tuashirie katika siku na Mwezi aliozaliwa ndani yake.

Imam Hassan al-Mujtaba (a.s), nasaba yake kwa upande wa Baba ni Mtoto wa Imam Ali (a.s),  na kwa upande wa Mama ni Mtoto wa Sayyidat Fatima (s.a) ambaye ni Binti yake Mtume Muhammad (s.a.w.w). Tizama nasaba hii!. Hapana shaka kuwa Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s) ni Mtoto Mtukufu, kutoka kwa Watu Watukufu, kuanzia Baba yake na Mama yake, na juu zaidi kuna Babu yake, ambaye ni Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), mbora wa viumbe vyote Duniani na Akhera.

Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s), alizaliwa (Tarehe 15) Usiku wa Nusu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mwaka wa 2 Hijria. Na hii ndio rai yenye nguvu zaidi inayofuatwa na Maulamaa wengi, na yenye ithibati zenye nguvu za kihistoria. (Sambamba na rai hiyo kuna rai nyingine ya pili isiyokuwa na nguvu isemayo kuwa alizaliwa katika Mwezi wa Shaaban).

Mwaka wa 2 Hijria, ambao alizaliwa ndani yake Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s), ndio mwaka ambao ilipiganwa ndani yake vita ya Badri. Na hii ni vita kubwa katika Historia ya Kiislamu, ambayo Waislamu waliuliwa sana katika vita hiyo, lakini mwisho wake Waislamu walitoka na Ushindi Mkubwa.

Muhammad bin Yaaqub Al-Kulayni (ra) anasema:

Alizaliwa Imam Hassan (a.s) ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, katika Mwaka wa vita vya Badri, ambao ni mwaka wa 2 baada ya Hijra ya Mtume (s.a.w.w). Na imepokewa pia kuwa alizaliwa katika mwaka wa 3 Hijria”.

Nukta ya msingi hapa ni hii kwamba: Sawa sawa iwe ni kauli ya wanaosema kuwa amezaliwa ndani ya mwaka wa 2 Hijria,  au kauli ya wale wasemao ilikuwa NI mwaka wa 3 Hijria, bado wote wanaafikiana kwa kauli moja kuwa ilikuwa ni ndani ya Nusu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

SEHEMU YA FADHILA ZA IMAM HASSAN AL-MUJTABA (A.S)

Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s) anazo fadhila nyingi na daraja ya juu

Imam Hassan Al-Mujtaba (a.s) anazo fadhila nyingi, itoshe katika sehemu hii kuashiria katika sehemu ya fadhila hizo, ambayo tunaikuta katika Hadithi Tukufu na maarufu ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) aliposema:

"إنّي تاركٌ فيكم الثقلين ما إن تَمَسَّكتم بهما لن تضلّوا بعدي: كتاب الله وعترتي أهلَ بيتي، لن يفترقا حتى يردا عليّ الحوضَ"

“Hakika mimi nimekuachieni vizito viwili, ambavyo ikiwa mtashikamana navyo, basi hamtapotea baada yangu, (navyo ni) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Itrah wangu Ahlul-Bayt wangu (Familiya yangu),  (vizito hivi viwili) havitokuja kutofautiana kamwe mpaka vitakaponirudia katika Haudhi”. Rejea ya Hadithi hii: (Al-Nasa’i, al-Sunan al-Kubra, 1411 H, juz. 5, uk. 45. al-Kulaini, al-Kafi, juz. 1, uk. 294).

Hadithi hii Tukufu iko wazi kwa watu wote wenye mazingatio. Haihitajii akili kubwa sana kuweza kuielewa Hadithi, na wala haihitajii ujanja ujanja wa kuitia ufundi na kuibadilisha ibara zake kwa sababu zozote zisizoeleweka na ambazo hatima yake ni mbio za sakafuni huishia ukingoni.

Mtume (s.a.w.w) anatutaka baada yake tushikamane Qur’an Tukufu na Ahlul-Bayt (a.s) katika mambo ya Dunia yetu na Akhera yetu, ikiwa hatutaki kupotea. Kwa maana kwamba: Kuamua kutokushikamana na vizito hivi viwili (Qur’an na Ahlul-Bayt -a.s-), hatimaya yake ni kupotea na kuwa mbali na njia sahihi inayoelekezwa na Qur’an na Ahlul-Bayt wa Mtume (amani iwe juu yao).

Tunayo mengi ya kujifunza kutoka ndani ya Qur’an Tukufu na kutoka kwa Itrah wa Mtume, Ahlul-Bayt wake Watoharifu (amani iwe juu yao), ambavyo ndio vizito vyetu viwili na viongozi wetu baada ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w). Na kumsoma na kumzungumzia Imam Hassan Al-Mujtaba (s.a), na kujifunza mengi kutoka kwake juu ya Uislamu wetu na Maisha yetu, ni sehemu ya kushikamana kisawa sawa na Ahlul-Bayt (a.s), ambao ndio kizito cha pili kwa ukubwa baada ya Qur’an Tukufu.

Na kuna rehma nyingi katika kujifunza ilmu na maarifa ya Imam Hassan al-Mujtaba (a.s), na Maimam watukufu wa Ahlul-Bayt (a.s), na kisha kuwafundisha watu ilmu na maarifa hayo. Mwenyezi Mungu atujalie tuwe miongoni mwa wale walioshikamana na vizito viwili (Qur’an Tukufu na Ahlul-Bayt -a.s-), na wakajifunza elimu na maarifa yao na kuyafikisha kwa watu.

Wassalam Alaikum Warahmatullah wa Barakatuh.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha