Vikosi vya usalama vya Afghanistan vimeanzisha operesheni dhidi ya wapiganaji wa jimbo la mashariki, eneo linaloonekana kuwa ngome ya kundi la Taliban, lililofanya mashambulizi ya mauwaji kwenye shule ya jeshi wiki iliyopita. Baada ya shambulizi hilo la Peshawar lililowaua watu 149, mkuu wa jeshi la Pakistan, Jenerali Raheel Sharif, alikutana na Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani mjini Kabul. Sharif alikuwa akitafuta kuungwa mkono na Ghani katika kupambana na kundi la Taliban nchini Pakistan, Tehreek-e-Taliban-TTP. Naibu msemaji wa wizara ya ulinzi, Dawlat Waziri, amesema vikosi vya Afghanistan vimeanzisha operesheni ya pamoja dhidi ya wapiganaji kwenye maeneo kadhaa ya wilaya ya Dangam. Amesema hadi sasa katika operesheni hiyo, wapiganaji 21 wenye silaha wameuwa na wengine 33 wamejeruhiwa na maafisa saba wa usalama wamejeruhiwa. Inaaminika kuwa kiongozi wa TTP, Mullah Fazlullah, amejificha kwenye mji wa Kunar, Afghanistan, unaopakana na Pakistan.