3 Juni 2019 - 06:16
UN: Zaidi ya raia 90 elfu wamekuwa wakimbizi kutokana na mapigano ya Tripoli, Libya

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu 90 elfu wamekuwa wakimbizi huko Tripoli, mji mkuu wa Libya tangu Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji huo mwezi Aprili mwaka huu.

(ABNA24.com) Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu 90 elfu wamekuwa wakimbizi huko Tripoli, mji mkuu wa Libya tangu Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji huo mwezi Aprili mwaka huu.

Televisheni ya "Rusia al Yaum" imemnukuu Farhan Haq, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akisema kuwa, idadi ya watu waliokimbia makazi yao mjini Tripoli, Libya, kutokana na mapigano, imeongezeka na kupindukia 90 elfu. Idadi yao inazidi kuwa kubwa siku baada ya siku kiasi kwamba katika kipindi cha wiki moja ya hivi sasa, karibu watu elfu nane wamekimbia makazi yao huku nusu yao wakiwa ni watoto wadogo.

Ameongeza kuwa, maafisa wa misaada wanaendelea na zoezi la kuwasaidia wakimbizi hao kiasi kwamba watu zaidi ya 47 elfu wa Tripoli na maeneo ya karibu na mji huo wameshafikishiwa misaada ya maafisa hayo.

Tarehe 4 Aprili mwaka huu Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri ya kushambuliwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Jenerali huyo muasi anaungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa. Hata rais wa Marekani, Donald Trump alimpigia simu jenerali huyo akitangaza uungaji mkono wake kwa kile alichodai ni kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa visima vya mafuta vya Libya.




/129