7 Oktoba 2022 - 20:55
Wizi wa miaka 9 katika bomba la kuuza mafuta ya Nigeria nje ya nchi

Serikali ya Nigeria Nigeria imegundua uuganishaji haramu katika moja ya vituo muhimu vya kuuza nje ya nchi mafuta ghafi ya petroli ya nchi hiyo.

Mkuu wa kampuni ya mafuta ya serikali NNPC LTD amesema wamegundua wizi wa mafuta kutoka kwenye mojawapo ya njia zake kuu za kusafirisha mafuta baharini na kuongeza kuwa wizi huo umekuwa ukiendelea kwa muda wa miaka tisa kabla ya kugunduliwa.

Bomba la wizi lina urefu wa kilomita 4 kutoka kwenye kituo cha usafirishaji cha Forcados, ambacho kwa kawaida husafirisha takriban mapipa 250,000 ya mafuta kwa siku. Mkuu wa NNPC Mele Kyari ameliambua bunge la Nigeria kuwa bomba hilo limegunduliwa baharini katika oparesheni ya kuzuia wizi katika wiki sita zilizopita.

Kyari amongeza kuwa, wizi wa mafuta ghafi ya petroli nchini humo umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya miaka 22 lakini haikudhaniwa kiwango hicho kilikuwa kikubwa kama ambacho kimegunduliwa hivi karibuni.

Mara nyingi wezi hupasua mabomba ya ardhini ili kufyonza mafuta bila kutambuliwa wakati wanaendelea kufanya kazi, lakini njia isiyo halali baharini si ya kawaida sana na inaonyesha operesheni ya wizi wa hali ya juu zaidi.

Nigeria ambayo ni muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi ya petroli barani Afrika hupoteza mapipa laki sita ya mafuta kwa siku kutokakna na wizi.

342/