Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:43:12
1323359

Tehran yalaani vikwazo vipya vya EU dhidi ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikwazo vipya vilivyotangazwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya shakhsia 29 na taasisi tatu za Kiirani, ikiwemo kanali ya televisheni ya Press TV.

EU ilitangaza vikwazo hivyo jana Jumatatu kwa tuhuma kuwa maafisa na taasisi hizo za Kiirani zimehusika na kukandamiza maandamano ya wananchi.

Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Tehran ina haki ya kujibu hatua hiyo ya nchi za Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Ameutaja uraibu huo wa vikwazo vya Wamagharibi kuwa uingiliaji wa mambo ya ndani ya taifa hili na ambao ni kinyume cha sheria, mbali na kuwa hauna maana yoyote.   

Usimamizi wa Press TV sambamba na kulaani vikwazo hivyo, umesema hatua ya Canada huko nyuma na Umoja wa Ulaya hivi sasa kuiwekea vikwazo kanali hiyo, inakanyaga uhuru wa kujieleza na kutoa mtazamo mbadala.

Katika hali ambayo Iran inaitakidi kuwa ghasia zinazoshuhudiwa hapa nchini ziliratibiwa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu nje ya nchi kama vile Marekani na waitifaki wake, lakini Mawaziri wa Mambo ya Nje wa EU waliokutana jana mjini Brussels walikuwa na mtazamo tofauti. Wakitangaza vikwazo hivyo, wamedai kuwa wafanya fujo nchini Iran wanapigania 'uhuru.' 

Maandamano ya kulalamikia kifo cha mwanamke wa Kiirani, Mahsa Amini yalianza katikati ya Septemba, lakini ghafla moja nchi za Magharibi zikayateka nyara na kuanza kuchochea moto wa fujo na ghasia nchini.

EU imetangaza kuwawekea vikwazo vya usafiri na kuzuia mali za shakhsia 29 wa Kiirani, akiwemo Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, askari polisi wanne wanaodaiwa kumtia mbaroni Amini, maafisa waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wakiwemo makamanda wa mikoani wa jeshi hilo, na vile vile Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Iran.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vipya licha ya serikali ya Rais Joe Biden kudai kuwa inakusudia kuandaa mazingira yanayohitajika kwa ajili ya kurejea nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kupitia mazungumzo.

342/