Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

8 Juni 2024

18:25:06
1464257

Bahrain imetuma salamu kupitia Russia za kutaka kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Iran

Afisa mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Bahrain imetuma salamu kwa Tehran kupitia Russia za kutaka kurejesha uhusiano wa kawaida baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya miaka minane.

Mohammad Jamshidi, Naibu Mkuu wa wafanyakazi wa masuala ya kisiasa wa Rais wa Iran, ameyasema hayo katika mahojiano na chaneli ya televisheni ya hapa nchini. Wiki iliyopita, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifah wa Bahrain alitangaza akiwa nchini China kwamba nchi yake inafanya juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani ya Iran.

"Tunaamini katika msingi wa ujirani mwema na kutoingilia mambo ya ndani," alieleza kiongozi huyo wakati wa mkutano na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing, ambako alikuwa katika ziara ya kiserikali, na akaongezea kwa kusema: "tunafanya juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Iran kama jirani".

Aidha, wakati wa mkutano wake na Rais Vladimir Putin wa Russia uliofanyika mjini Moscow Mei 23, Mfalme Hamad alisema Bahrain inatazamia kuboresha uhusiano wake na Iran.

Aliongeza kuwa, hakuna sababu ya kuahirisha kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Bahrain na Iran.

Bahrain iliifuata Saudi Arabia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 4, 2016, baada ya waandamanaji nchini Iran walioghadhibishwa na kunyongwa mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudia kuvamia jengo la ubalozi wa nchi hiyo hapa mjini Tehran.

Mnamo Machi 2023, Iran na Saudi Arabia zilifikia makubaliano katika mji mkuu wa China, Beijing ya kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi na ofisi zao za kidiplomasia.

Itakumbukwa kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain Abdullatif al-Zayani alitembelea Tehran hivi karibuni kutoa rambirambi kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi, ambaye alikufa shahidi pamoja na watu wengine saba katika ajali ya helikopta iliyotokea Mei 19 kaskazini-magharibi mwa Iran.

Katika mahojiano hayo ya televisheni Mohammad Jamshidi, amezungumzia makubaliano ya kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Iran na Saudi Arabia katika serikali ya Rais Ebrahim Raeisi na akasema: "Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuunga mkono, na kisha wakaunga mkono ndugu wa Muqawama wa nchini Yemen".

Jamshidi amebainisha pia kuwa Mwanamfalme wa Saudia Mohammad bin Salman naye pia aliomba kurejeshwa uhusiano wa nchi hiyo na Iran kupitia Rais Xi Jinping wa China, na akaongezea kwa kusema: "kadhalika, Bahrain imetuma salamu kwa Iran kupitia Russia za kutaka kurejesha uhusiano na Iran".../

342/