Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Ahmad Haji kupitia kipindi Maalum kila chorushwa live / mubashara na chaneli ya Haditv8 amechambua kwa kina umuhimu wa kujenga shakhsia na utu katika maisha ya kila siku ya Mwanadamu, akibainisha misingi muhimu inayopaswa kuzingatiwa ili kuimarisha maadili, mshikamano na haki katika jamii.
Katika maelezo yake, Sheikh Ahmad Haji amesisitiza kuwa Uislamu ni dini inayohimiza msamaha, haki na kujiepusha na dhulma katika nyanja zote za maisha. Ameeleza kuwa Muislamu anatakiwa kumsamehe aliyemkosea au aliyemdhulumu, huku yeye mwenyewe akihakikisha hamdhulumu mtu mwingine kwa kauli, vitendo au maamuzi yake.

Akifafanua zaidi juu ya athari mbaya za dhulma, Sheikh Ahmad Haji amesema kuwa jamii ya leo imejaa aina mbalimbali za dhulma, jambo linalohatarisha amani na uhusiano mwema baina ya watu. Ameonya kuwa dhulma haimaliziki bila madhara, kwani humfikisha mwenye kuitenda katika majuto makubwa hapa duniani na Akhera.

“Unaweza kumdhulumu mtu na ukalala usingizi mzito, lakini yule uliyemdhulumu halali kamwe. Anakumbuka dhulma yako kila siku na humlalamikia Mwenyezi Mungu dhidi yako. Na ikumbukwe kuwa macho ya Mwenyezi Mungu hayalali,” amesema Sheikh Ahmad Haji, akisisitiza hatari ya dua ya aliyedhulumiwa.

Ameongeza kuwa katika jamii tunamoishi, ni wajibu wa kila mmoja kumuogopa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na dhulma kwa hali na mali, kwani dhulma huvuruga amani ya jamii, huondoa baraka na huleta chuki, migogoro na maangamizi.

Sheikh Ahmad Haji amehitimisha kwa kuwakumbusha Waumini na jamii kwa ujumla kuwa kujenga shakhsia ya utu kunaanzia ndani ya nafsi ya mtu, kwa kuzingatia haki, huruma, msamaha na kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo, ili kuijenga jamii yenye haki, amani na maadili mema.

Your Comment