Main Title

source : Parstoday
Jumanne

16 Julai 2024

21:18:52
1472416

Iran ya Kiislamu yaghariki kwenye Tasua ya Imam Hussein AS

Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram wameshiriki katika vikao, marasimu, majlisi na shughuli mbali mbali za maombolezo ya Tasua ya Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume wetu Muhammad SAW.

Maashiki na wapenzi wa Imam Hussein AS katika kona zote za Iran ya Kiislamu, leo Jumatatu wameshiriki katika maombolezo ya Tasua kwa hamasa kubwa zaidi kuliko miaka ya huko nyuma. 

Waombolezaji katika kona zote za Iran wametangaza kwa sauti kubwa utiifu wao kwa wanamapambano wa Karbala, huku wakijibari na kujiweka mbali na maadui wa Uislamu na wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.

Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram, waombolezaji humkumbuka zaidi Abul Fadhl Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein AS ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashura. 

Alionesha ushujaa wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib (AS). Abul Fadhl Abbas aliuawa shahidi tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW ambao kinara wao alikuwa ni Yazid bin Muawiyah.

Katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran, majlisi za maombolezo na kuwakumbuka mashujaa wa Karbala hususan Abul Fadhl zimefanyika katika maeneo mbalimbali; huku marasimu makubwa yakifanyika jana usiku katika Husseiniya ya Imam Khomeini MA, ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei alishiriki pia.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa Waislamu wote hususan Mashia na wapenda uhuru wengine duniani kwa mnasaba wa siku hii ya Tasua ya Imam Hussein (AS).

342/