Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo katika mkutano wake na wajumbe wapya wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Pendekezo langu kubwa ni kuwepo maingiliano athirifu kati ya Bunge na serikali mpya. Mafanikio ya Rais na serikali mpya ni mafanikio yetu sisi sote. Kila mmoja ana wajibu wa kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake kwa taifa."
Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa: Rais akifanikiwa kusimamia mambo ya nchi, kuboresha uchumi, kuendeleza mahusiano ya nchi za nje na masuala ya kiutamaduni, sote tunafanikiwa. Ushindi wake ni ushindi wetu sote.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amewataka wabunge na viongozi wengine wa Iran kuwa na sauti moja katika kushughulikia masuala muhimu ya nchi, ili kuwakasirisha wanaotaka kupanda mbegu za mifarakano miongoni mwao.
Amewaasa Wabunge kulipasisha haraka Baraza jipya la mawaziri ambalo litatangazwa karibuni na Dakta Pezeshkian na kuongeza kuwa, "Kadri baraza jipya la mawaziri litakavyopitishwa haraka na serikali ianze kufanya kazi, ndio bora kwa nchi."Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameeleza bayana kuwa, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) inaweza kuwa na nafasi kubwa katika kuondolewa na kuzimwa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kubainisha kuwa: Kadhia ya Gaza linasalia kuwa suala kuu la umma wa Kiislamu.
Ameeleza kuwa: Vyombo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kijeshi 'vinavyoitwa Marekani' pamoja na utawala ghasibu wa Kizayuni vinapigana na kundi dogo liitwalo Muqawama, na kwa kuwa waovu hawa wawili (Marekani na Israel) hawajafaulu kuisambaratisha (Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina) Hamas na Muqawama, wanashambulia kwa mabomu hospitali, shule, watoto, wanawake na watu madhulumu wa Gaza.
342/