Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Julai 2024

16:28:09
1473821

Iran na Sudan zarejesha uhusiano; balozi wa Iran Khartoum akabidhi hati za utambulisho

Kiongozi wa Baraza la Utawala wa Mpito na Mkuu wa Majeshi ya Sudan, Abdul Fattah Al-Burhan, amepokea hati za utambulisho za balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sudan, Hassan Shah Hosseini.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan kwa vyombo vya habari imesema kwamba, balozi wa Iran jana aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Abdel Fattah Al-Burhan Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan jambo linaloashiria kwamba, kiongozi huyo amemkaribisha balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sudan.

Al-Burhan amesisitiza kuimarika kwa uhusiano kati ya Sudan na Iran na kueleza kuwa, uwasilishaji wa hati za utambulisho za balozi huyo unaashiria mwanzo wa awamu mpya ya mchakato wa uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo mbili.Kwa upande wake balozi mpya wa Iran nchini Sudan amesema kuwasilisha hati zake za utambulisho kunakuja ndani ya fremu ya maafikiano ya pamoja kati ya nchi hizo mbili kuhusu kubadilishana mabalozi na kukuza uhusiano wa pande mbili, na kusisitiza kuwa atafanya kila juhudi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Sudan.

Hassan Shah Hosseini amesisitiza kuwa, nchi yake inaunga mkono mamlaka ya kitaifa, umoja na amani ya Sudan. Uhusiano wa Sudan na Iran umerejea baada ya kupita miaka minane wakati Khartoum ilipochukua hatua ya kukata uhusiano wake na Tehran.


342/