Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

8 Agosti 2024

15:09:36
1477382

Ofisi ya Kudumu ya I.R.Iran UN: Iran itaifanya Israel ijutie uchokozi wa kigaidi iliofanya

Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imesema Tehran itaufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ujutie kitendo cha uchokozi wa kigaidi uliofanya hivi karibuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu uliopelekea kuuawa shahidi kiongozi mkuu wa Hamas, Ismail Haniya.

Ofisi hiyo ya uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika UN ilitoa kauli hiyo jana Jumatano wakati wa kujibu masuali kuhusu madai kwamba Tehran inaweza ikafuta kisasi chake ikiwa Tel Aviv itafikia makubaliano na Hamas ambayo yataleta suluhu katika vita vinavyoendelea vya utawala huo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Ghaza. "Tumekuwa tukifuatilia vipaumbele viwili kwa wakati mmoja," imeeleza ofisi hiyo ya uwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa na kufafanua kwa kusema: "kwanza, kufikiwa usitishaji vita thabiti huko Ghaza na kuondolewa wavamizi katika eneo hilo. Na pili ni kutoa adhabu ya mvamizi kwa mauaji ya Shahidi Haniya, kuzuia kurudiwa kwa vitendo vya uchokozi vya utawala wa Kizayuni, na kuwafanya Wazayuni wajutie kujiingiza kwenye mkondo huu".Mapema jana Jumatano, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani alirudia na kutilia azma iliyonayo Jamhuri ya Kiislamu ya kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni.

 Bagheri, ambaye alikuwa akihutubia kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Jeddah, Saudi Arabia alisema Tehran haina chaguo jengine isipokuwa kulipiza kisasi dhidi ya utawala huo kutokana na mauaji hayo na kuongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuzuia uchokozi zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekaa bila ya kuchukua hatua yoyote.../


342/