Jumapili asubuhi, vyanzo vya habari viliripoti kwamba kombora la Yemen lilipiga eneo la karibu na Tel Aviv na moto ukazuka baada ya hapo. Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa Jeshi la Yemen, huku akifafanua operesheni hiyo ya kipekee ya kombora amesema kuwa tukio hilo limetokea kwa mara ya kwanza katika historia bandia ya adui Mzayuni. Amesema katika taarifa kwamba operesheni hiyo dhidi ya Tel Aviv ambayo imefanywa kwa kombora jipya la balistiki la Hypersonic, imefikia lengo lake na kwamba mifumo ya ulinzi ya adui alishindwa kulizuia. Ameongeza kuwa kombora hilo lilisafiri umbali wa kilomita 2,040 kwa muda wa dakika 11 na sekunde 30, ambapo liliwasababishia Wazayuni kiwewe na hofu kubwa na kupelekea zaidi ya milioni mbili kati yao kukimbilia mafichoni chini ya ardhi, na kuwa tukio hilo lilikuwa la kwanza kutokea katika historia ya Wazayuni.
Kwa kutilia maanani matamshi hayo ya msemaji wa Jeshi la Yemen, tanapasa kuashiria hapa nukta hii kuwa operesheni ya Jumapili imethibitisha wazi kwamba Wayemen wamefikia teknolojia na ujuzi mkubwa wa kijeshi wa kutengeneza kombora la Hypersonic na hivyo kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo kwa manufaa ya mhimili wa muqawama ambapo haya yote yamepatikana licha ya vita na vikwazo vya miaka 9 na mzingiro wa kiuchumi wa maadui dhidi ya taifa la Yemen.
Nukta nyingine muhimu kuhusu operesheni ya Jumapili ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ni kutokuwa na uwezo wa mfumo wa ulinzi wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kulizuia kombora hilo. Wayemen walirusha kombora moja tu kuelekea Tel Aviv, ambalo lilisafiri umbali wa kilomita 2,040 bila kuzuiliwa. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, kombora hilo lilipiga njia ya reli ya Tel Aviv kuelekea Quds Tukufu, karibu kilomita 6 kutoka mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Sayyid Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah amesema kuhusiana na suala hilo kwamba operesheni ya Jumapili ilifanywa kwa kombora la hali ya juu kabisa, kusafiri umbali wa kilomita 2,040 na kukwepa mifumo ya ulinzi ya adui kwa mafanikio makubwa.
Operesheni ya Jumapili ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeanika wazi udhaifu mkubwa wa utawala wa Kizayuni. Vyanzo vya Kizayuni vimesema kuwa, ijapokuwa shambulio la Yemen lilitekelezwa kwa kombora moja tu, lakini lilipelekea idadi kubwa ya wakaazi wa mji mkuu na miji ya jirani kukimbilia mafichoni. Hivyo, ukosefu wa usalama na hofu kwa walowezi wa ardhi za Palestina imeangaziwa tena kwa kiwango kikubwa.