20 Septemba 2024 - 20:13
Mbunge Mmarekani Mpalestina alikabidhi Bunge la US orodha ya majina ya watoto waliouliwa Ghaza

Mbunge Muislamu wa Marekani mwenye asili ya Palestina Rashida Tlaib amewasilisha mbele wa Bunge la Marekani kwa ajili ya kuwekwa kwenye kumbukumbu majina ya watoto wa Kipalestina waliouliwa na jeshi dhalimu la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Majina hayo yamenakiliwa kutoka kwenye orodha ya kurasa 649, iliyochapishwa hivi majuzi na Wizara ya Afya ya Ghaza. "Kurasa 14 za kwanza pekee ni majina ya watoto [ambao] walikuwa na umri wa chini ya mwaka mmoja walipouawa," amesema Tlaib, ambaye ni mbunge pekee wa Marekani mwenye asili ya Palestina ndani ya Kongresi. Tlaib amefafanua kwa kusema: "hao ni watoto 710 ambao serikali ya Israel imewaua. Natamani wenzangu waiangalie. Huku si kujilinda. Haya ni mauaji ya kimbari”.

Wizara ya Afya ya Ghaza siku ya Jumatatu ilichapisha ripoti inayoelezea jina, umri, jinsia na namba za utambulisho za makumi ya maelfu ya watu waliouliwa na jeshi la Israel katika kipindi cha miezi 11 iliyopita tangu utawala huo wa Kizayuni uanzishe vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Hati hiyo ya kutisha yenye kurasa 649 ina maelezo ya Wapalestina 34,344 waliouawa kufikia Agosti 31, huku mchakato wa kukusanya data wa karibu watu 7,000 zaidi ukiendelea.

Kurasa 11 za mwisho za ripoti ya Wizara ya Afya ya Ghaza zinaorodhesha Wapalestina wenye umri wa miaka 77 hadi 101, ambao wote walizaliwa kabla ya kuanzishwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 kwenye ardhi ya Palestina iliyonyakuliwa.

Ripoti ya Julai ya jarida la matibabu la Uingereza, The Lancet ilikadiria kuwa uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Ghaza unaweza ukawa umesababisha idadi kubwa ya vifo vya Wapalestina vya kati ya watu 149,000 na 598,000 ikiwa vita vingemalizika wakati huo.../

342/