Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Beirut | Amin Sherri, kiongozi mwandamizi wa Hezbollah na mbunge wa muungano wa “Uaminifu kwa Muqawama” katika Bunge la Lebanon, amesema kuwa hadi sasa hakuna uthibitisho wowote rasmi kuhusu safari ya Ammar Al-Moussawi, afisa wa mahusiano ya kigeni wa Hezbollah, kwenda Saudi Arabia. Amesisitiza kuwa ni lazima kusubiri tamko rasmi kutoka Riyadh au kutoka ofisi ya habari ya Hezbollah.
Sherri alisisitiza msimamo usiobadilika wa Hezbollah akisema kuwa mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Kizayuni yanamaanisha kutoa masharti zaidi kwa upande wa Lebanon, na kwamba Lebanon haiwezi kupata faida yoyote kutoka Tel Aviv.
Mbunge huyo alitoa wito wa majadiliano ya kitaifa ya ndani ili kufikia msimamo mmoja wa kitaifa, akibainisha kuwa kipaumbele kinapaswa kuwa kulinda uhuru wa taifa kupitia kuikomboa ardhi iliyokaliwa, kuwaachia huru wafungwa, na kusitisha uvamizi wa Israel.
Alikumbusha kuwa Hezbollah hapo awali ilitoa wito wa mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuandaa mkakati wa ulinzi wa taifa, lakini haikupata mwitikio, huku akisisitiza kuwa chama hicho bado kiko tayari kwa maelewano na pande zote za Lebanon.
Sherri alieleza kuwa utekelezaji kamili wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1701 ni jukumu la kipekee la serikali ya Lebanon, akiongeza kuwa Hezbollah inasisitiza serikali itekeleze majukumu yake yote ya ulinzi na usalama.
Pia alithibitisha ushirikiano kamili wa Hezbollah na Jeshi la Lebanon katika mpango wa kupeleka vikosi vya jeshi kusini mwa Mto Litani, lakini akaonesha mashaka juu ya uzito wa uungaji mkono wa kimataifa kwa jeshi hilo—hasa baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa misaada ya jeshi mjini Paris hadi mwezi Februari.
Mbunge huyo wa Hezbollah alifichua kuwa balozi wa zamani wa Marekani alimwambia mmoja wa mabalozi wa Kiarabu kwamba kila silaha iliyo mikononi mwa Hezbollah inapaswa kuharibiwa baada ya kunyang’anywa au kuuzwa nje ya nchi.
Kuhusu uwezekano wa Lebanon kujiunga na Mikataba ya Abraham, Sherri alisisitiza kuwa uamuzi huo ni haki ya watu wa Lebanon pekee, ambao wanafahamu kuwa aina yoyote ya ukaribu na Israel inatishia uwepo wa Lebanon kwa mujibu wa mradi wa “Israel Kubwa”. Aliongeza kuwa jukumu la Marekani ni kuhakikisha usalama wa kimkakati wa Israel katika eneo zima, hususan Lebanon na Syria.
Sherri alitangaza pia kuwa Hezbollah imefanya tathmini ya kina ya uharibifu wa vita, na kukadiria gharama za ujenzi upya (bila kujumuisha taasisi za kibiashara) kufikia dola bilioni 4 za Marekani.
Katika masuala ya uchaguzi, alisema Hezbollah iko tayari kushiriki uchaguzi wa bunge, lakini inasisitiza ufanyike katika muda wa kisheria, yaani tarehe 3 Mei. Aidha, alifichua kuwa mawaziri wa mambo ya nje na mambo ya ndani hawajatoa maelezo yoyote kuhusu vikwazo vya kufanyika kwa uchaguzi katika eneo la 16 (Wale Lebanoni wanaoishi nje ya nchi).
Ikumbukwe kuwa jarida moja la Lebanon lilidai hivi karibuni kuwa Ammar Al-Moussawi, afisa wa mahusiano ya kigeni wa Hezbollah, amekuwa kwa siku tatu katika safari ya siri nchini Saudi Arabia kwa upatanishi wa Uturuki, madai ambayo hadi sasa hayajathibitishwa rasmi.
Your Comment