27 Januari 2021 - 11:28
Tahadhari ya wimbii jipya la Corona yatanda nchini Tanzania

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania limewataka Watanzania kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya virusi vya Corona wakati huu dunia ikikabiliwa na janga hilo la kiafya ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka misongamano.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kupitia waraka wake uliosainiwa na Rais Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Baraza hilo la maaskofu limesema, hata kama Tanzania hakuna ugonjwa COVID 19, bado wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari za kiafya ili kujikinga na virusi vya Corona kwa sababu Tanzania sio kisiwa.

Wakati huo huo, Viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania wamezungumzia janga la virusi vya Corona linalokabili dunia na kutoa wito kwa wizara husika kutoa tamko juu hali ya afya nchini humo.

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe amesema umefika wakati kwa Wizara ya Afya kutoa tamko kuhusu janga hilo linalosumbua dunia na nchi jirani.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha Chadema, Freeman Mbowe amewataka madaktari kupitia kiapo chao kueleza hali halisi na hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waziri wa Fedha na Mipango, wa Tanzania Dakta Philip Mpango amenukuliwa akiwataka wafanyakazi wa wizara kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 ingawaje ugonjwa huo haupo nchini humo.

Tanzania haijatoa takwimu za maambukizi ya Corona tangu mwisho wa mwezi Aprili mwaka 2020, na rais John Magufuli amekuwa akisema maombi yameisaidia nchi hiyo kuondokana na janga hilo.

Wiki iliyopita, Uingereza iliwazuia abiria kutoka nchini Tanzania kwenda nchini humo kwa hofu kuwa watasambaza aina mpya ya virusi vya Corona.

342/